Thursday, April 20, 2017

MWANASHERIA MKUU- UZOEFU WA MAWAZIRI NI WAKASI KUBWA

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, George Masaju ametetea uzoefu wa viongozi katika serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, John Magufuli, tofauti na hoja za kambi ya upinzani bungeni kuwa serikali haina uzoefu.

Masaju akijibu hoja za wabunge bungeni jana, alisema inashangaza kuona wapo wanaodai serikali haina uzoefu, ilhali mambo yanakwenda kwa kasi kiasi cha kupigiwa makofi ndani ndani na nje ya Afrika.

“Halafu kuna hoja imezungumzwa jana ni aibu, unasema serikali hii inaongozwa na watu wasio na uzoefu, hili linawezekanaje? Rais mwenyewe amekuweko bungeni tangu mwaka 1995 na mawaziri wanaomsaidia walikuwepo hapa sisi watumishi wa umma tumekuwepo humu mimi nimeanza kazi mwaka 1994. “Kinachobadilika ni wanasiasa na nyie wenyewe mlienda katika kura mkashindanishwa msio na uzoefu na walio na uzoefu, walio na uzoefu wakashinda na wameunda serikali mnasema they are not competent, this is not serious at all, we need to be serious.

Huyu rais mnayemsema mimi nilikuwepo pale ubungo mwezi jana kwenye ujenzi wa barabara sijui mnaita madaraja, yule Rais wa Benki ya Dunia (Dk Jim Yong Kim) alisema alikuja Tanzania kwa sababu huko duniani viongozi wanasema nenda Tanzania kwanza. Mnataka uzoefu wa aina gani?” alisema. Aliendelea kusema kuwa, Serikali ya Rais Magufuli inaongozwa na watu wanaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi ipasavyo, na ndio maana imeweza kutekeleza mambo mengi ya msingi ndani ya muda mfupi.

“Mwenye macho haambiwi tazama,” alisema na kushauri bila ya ushirikiano baina ya viongozi wa serikali na wale wa upinzani, mambo hayawezi kwenda sawa. Katika kukazia hoja yake, alisema: “Ushirikiano mnaoutaka na serikali lazima uanzie humu bungeni uta extend hadi majimboni kwenu, hamuwezi kuwa mnawatukana mawaziri halafu kesho mnamwambia aje jimboni kwako.

Unasema kwamba waziri hayuko competent sasa unamuitia nini jimboni? Kufanya nini? Tusiruhusu watu wachache wakaharibu amani ya taifa hili kama kwa vitendo ama kwa kauli zao ama kwa nyendo zao, lazima turudishe nidhamu ndani ya bunge hili. Bunge ‘Live’ Akizungumzia suala la wabunge kulilia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kama ilivyokuwa hapo awali, Mwanasheria Mkuu aliwataka wabunge kutambua kuwa, kinachotakiwa ni kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha ili waendelee kukubalika kwa wananchi wao.

Alisema Serikali haijakataza vyombo vya habari kutoa taarifa kwa umma, bali kilichofanyika ni mabadiliko tu ya utaratibu, ndiyo maana vyombo kama magazeti havijazuiliwa kuripoti mambo yanaendelea bungeni. Aliongeza kuwa, kama `Bunge Live’ lingekuwa suluhisho la kutambulika kwa kazi za wabunge, basi asilimia zaidi ya 70 ya wabunge walioanguka katika uchaguzi wa mwaka 2015 wasingepata anguko hilo la kisiasa, kwa kuwa matangazo yalikuwa yanarushwa moja kwa moja. “Naomba kushauri kuwa tusitumie vibaya uhuru wa mijadala.

Na hata huku kutangazwa inaitwa matangazo mubashara, someni ibara ya 100 kama ipo hiyo haki someni sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge kama iko hiyo haki. Someni kanuni 143 haki tuliyonayo ni taarifa za bunge ibara ya 18 ya katiba inatoa haki ya watu kupewa taarifa. “Niwashauri waheshimiwa wabunge kama mtataka kurudi kwenye bunge hili, teteeni mambo yanayowahusu wapiga kura wenu, matangazo mubashara hayawasaidii chochote,” alisema.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka wenye taarifa kuhusu kupotea kwa aliyekuwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane washirikiane na jeshi la Polisi ili kufanikisha kupatikana kwake. “Wenye taarifa wakiwemo waliokuwa wakifanya naye kazi watoe ushirikiano kwa polisi ili kuweza kupata ufumbuzi wa hili na kujua alipo Sanane,”alisema.

Mbali na hilo, aliwataka wabunge kutoutumia vibaya uhuru unaotokana na nyadhifa zao. Alisema ingawa wabunge wanapewa uhuru wa kuzungumza wawapo bungeni, lakini wanapaswa kuchunga mipaka na haki za wengine katika kuwasilisha na kushughulikia mambo mbalimbali yaliyo kwenye nyadhifa zao.

No comments:

Post a Comment