KUREJEA kwa beki kiraka, Abdi Banda kumempa matumaini Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog ya kuwaondoa wapinzani Azam FC watakaopambana nao Jumamosi hii kwenye mechi ya Kombe la FA, hatua ya nusu fainali.
Banda amerejea kikosini hivi karibuni akitoka kifungoni baada ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirisho la Soka Tanzania (TFF) kumfutia adhabu kwa kosa la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla.
Awali, Banda alisimamishwa na Kamati ya masaa 72 ya Shirikisho ambayo alikosa michezo miwili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Akizungumza na Championi Jumatano, Omog alisema kuwa anafurahi kuona beki wake ambaye ni tegemeo akirejea uwanjani kwenye mechi dhidi ya Azam baada adhabu yake kufutwa.
Omog alisema, kwenye mechi mbili ambazo beki huyo hakuwepo pengo lake lilionekana kutokana na umuhimu wake mkubwa kwenye kikosi chake kilichopanga kuchukua mataji mawili ya ligi kuu na Kombe la FA. “Sina hofu na kikosi changu kuelekea mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA tutakapokutana na Azam Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, kwani nina furaha ya kurejea kwa Banda.
“Kama unavyojua Banda alikosa michezo miwili ya ligi kuu dhidi ya Mbao tuliowafunga mabao 3-2 na Toto African ambayo tulitoka suluhu, hivyo nina imani kubwa ya kupata ushindi kwenye mchezo huo. “Ninafahamu mechi itakuwa mgumu sana, lakini kwa upande wetu Simba tumejiandaa vema kwa ajili ya mchezo huo na tayari tumeziboresha baadhi ya nafasi zenye upungufu kuhakikisha tunavuka kisiki hiki cha kwanza tukisubiria ligi kuu,” alisema Omog.
No comments:
Post a Comment