JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Joaquine De-Mello ameamuru
mtuhumiwa wa mauaji ya mwanawe kwa kutumia nyundo na ambaye ni mchinja
nguruwe, Ezekiel Magige akapimwe akili Dodoma.
Magige, ambaye ni mkazi wa mji mdogo wa Sirari alifikishwa mahakamani
jana kwa tuhuma za kumuua mtoto wake kwa kumpiga kwa nyundo kichwani na
ubongo kusambaa.
Mahakama Kuu ipo katika vikao vyake vya kikanda Tarime kwa wiki mbili na
Jaji De-Mello anasaidiwa na Jaji Rose Ebrahim. Kesi zaidi ya 40 ama
zitatajwa au kusikilizwa, zikihusisha makosa ya mauaji, madawa ya
kulevya na ujambazi wa kutumia silaha.
Wakili wa Serikali, Harry Mbogoro alidai kuwa Desemba 28, 2014 na akiwa
nyumbani kwake Sirari, mtuhumiwa Magige alimpiga kwa nyundo kichwani
mwanawe Julias Michael na kusababisha kifo chake papo hapo.
Jaji De-Mello alisema "ninaagiza mtuhumiwa huyu Ezekeil Magige apelekwe
Isanga Dodoma kupimwa akili kabla ya kusikilizwa kwa kesi yake kwani
tukio hili sio la kawaida.
" "Mtu mwenye akili timamu (anaweza) kumuua mtoto wake kwa kumpiga kwa
nyundo kichwani mtoto wake hadi ubongo kusambaa?" Katika kesi nyingine,
mfanyabiashara Tumaini Wankyo (28) alihukumiwa kwenda jela mwaka mmoja
baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia.
Wankyo alikuwa ameshitakiwa kwa kumuua bila kukusudia askari Jeshi la
Wananchi, Rojar Elias kwa kumpiga risasi, wakati wakigombea mwanamke
hotelini.
Katika kikao cha Mahakama Kuu kwenye Mahakama ya Wilaya Tarime, Wakili
Mbogoro alidai kuwa mauaji hayo yaliyokea Agosti 17, 2015 saa 7 usiku
katika Hotel ya NK iliyopo mjini Tarime.
Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa akiwa na mpenzi wake wa kike wakila chakula na
vinywaji, alifika askari Elias akiwa na wenzake wawili na kutaka
kumchukua mwanamke huyo kwa nguvu.
Ilielezwa kuwa katika kutekeleza azma hiyo, Elias alimshambulia Wankyo
kwa kumpiga ngwara na kumwangusha chini akiwa na bastola iliyokuwa na
risasi kwenye chemba.
Wakili wa Serikali Mbogoro alidai katika purukushani hiyo risasi moja
ilichomoka kutoka kwenye bastola ya Wankyo anayomiliki kihalali na
kumjeruhi askari huyo ambaye alifariki akipatiwa matibabu Hospitali ya
Bugando, Mwanza. Jaji De-Mello alimuhukumu kwenda jela mwaka mmoja.
No comments:
Post a Comment