Serikali imebariki vyama vya michezo mingine visiwani Zanzibar kujitegemea kimataifa kama walivyofanya wenzao wa soka.
Kauli ya Serikali imekuja siku chache baada ya visiwa hivyo kupata uanachama wa kudumu kwenye Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeshauri vyama
vingine vya michezo kuanza utaratibu wa kuiombea Zanzibar uanachama wa
Afrika ili ishiriki mashindano ya Afrika kama nchi.
“Katika masuala ya Muungano, sekta ya michezo haikujumuishwa ndiyo
sababu Zanzibar ina baraza lake la michezo (BMZ) na kurugenzi ya
maendeleo ya michezo,” alisema Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja na
kuongeza.
“Tulikuwa tukitumia majadiliano katika uteuzi wa timu pale tunapojiandaa
na Michezo ya Afrika au Michezo ya Jumuiya ya Madola na hata Michezo ya
Olimpiki, lakini kipindi hicho hutawaliwa na vurugu kweli kweli kwani
kila mmoja huvutia kwake.
“Huu ni wakati sasa wa vyama vingine vya michezo navyo kuamua kuiombea
Zanzibar uanachama wa Afrika ili ishiriki kama nchi kwenye michezo
mingine mbali na soka,” alisema Kiganja.
Wakizungumzia harakati kama zitawezekana, Mwenyekiti wa Chama cha
Netiboli Tanzania (Chaneta), Anna Kibira na Katibu Mkuu wa Kamati ya
Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi walionyesha mtizamo hasi juu ya
mpango huo.
“Soka walioamua kujitenga waache wafanye hivyo wao wana maslahi yao,
lakini Chaneta na Chaneza tutaendelea kuungana kimataifa, sisi ni wamoja
halafu mambo haya sitaki kuyazungumzia zaidi kwani ni ya kisiasa,”
alisema Kibira.
Bayi kwa upande wake alisema hana hoja katika hilo kwani ni suala la
kisiasa zaidi kuomba uanachama wa Afrika au kuungana na ule wa dunia.
No comments:
Post a Comment