Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema watakwenda
bungeni kupinga bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2017/18 kwa kuwa
haitekelezeki.
Amesema mapendekezo ya bajeti hiyo ya Sh31.6 trilioni yaliyowasilishwa
juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango hayawezi
kutekelezeka kwa sababu hata ya mwaka huu wa fedha ni asilimia 34 ya
fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo zimetolewa.
Akifungua mkutano wa Baraza la Uongozi la Chadema Kanda ya Kaskazini
uliofanyika jijini hapa, Mbowe (pichani) alisema katika kikao cha kamati
kuu ya chama hicho kilichofanyika jana wameweka msimamo kuwa bajeti
hiyo haina msaada wowote kwa wananchi hasa wa hali ya chini.
“Kambi ya upinzani bungeni tunakwenda kupinga bajeti hiyo kwa sababu
tunaamini fedha hizo hazitapatikana kwa ajili ya kutekeleza miradi ya
maendeleo,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alisema mwaka jana wabunge wa kambi ya upinzani
walieleza wazi kwamba bajeti ya mwaka huu isingetekelezeka na ndivyo
ilivyotokea kwa sababu kati ya Sh11.8 trilioni zilizotengwa kwa shughuli
za maendeleo ni Sh3.97 trilioni pekee zilizotolewa ikiwa ni asilimia 34
pekee.
“Angalau hata ingefikia asilimia 75 kungekuwa na matumaini, lakini hali
halisi inaonyesha Serikali haina fedha na imeweka bajeti bila kuangalia
uhalisia, matokeo yake hadi kipindi cha mwaka wa fedha kinamalizika
halmashauri zinajikuta hazijafikishiwa fedha za kutekeleza shughuli za
maendeleo,” alisema Mbowe.
Mbali ya bajeti, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, alitoa rai
kwa Rais John Magufuli kuhusu hali ya kisiasa nchini akieleza kwamba
baadhi ya matamko yanaweza kuwakimbiza wawekezaji, hivyo kusababisha
kuporomoka kwa uchumi.
Pia alizungumzia suala la utoaji na upatikanaji wa taarifa akisema
“Ushauri wa bure, Rais awaache wananchi wazungumze, anastahili
kusikiliza vilio vya wananchi wake, awe mwepesi kusikiliza kuliko
kujibu. Wananchi wasiposema mawe yatasema.”
Chadema ni Maalim Seif
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alieleza msimamo
wa chama hicho uliowekwa katika kikao cha Kamati Kuu kuwa kinamtambua
Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ndiye katibu mkuu wa CUF na
hakitashirikiana na Magdalena Sakaya.
“Tunatambua kuwa Profesa Ibrahim Lipumba amepewa jukumu la kuiua CUF,
sisi Chadema hatuwezi kukubali kwa kuwa itaua Ukawa na baadaye Chadema,”
alisema Mnyika.
Alisema chama hicho kitapambana kuhakikisha CUF haipasuki.
No comments:
Post a Comment