MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya inawashikilia,
kuwahoji na kuwachunguza vigogo watano walio katika orodha ya watu 97
wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo, waliokabidhiwa na serikali ya mkoa
wa Dar es Salaam.
Hatua hiyo ilibainishwa jana jijini humo na Kamishna wa Intelijensia wa
mamlaka hiyo, Fredrick Kibuta, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwaka
2016 ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.
Ufafanuzi huo ulikuja baada ya waandishi wa habari kutaka kujua hatua
zilizochukuliwa baada ya mamlaka kukabidhiwa orodha hiyo mapema mwezi
uliopita.
Majina ya wanaodaiwa kuwa ni vigogo, watoto wa viongozi na
wafanyabiashara wakubwa wa mihadarati ilikabidhiwa kwa Kamishana Mkuu wa
Mamlaka, Rogers Sianga na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,
siku mbili baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli, Februari 10.
Majina hayo, alidai Makonda, ni ya watu wanaohusika na biashara ya mihadarati tangu utawala wa awamu ya pili hadi ya tano.
“Tumekamata watu watano ambao ni muhimu sana katika mapambano ya dawa za
kulevya, na wengine wengi tunawahoji," alisema Kibuta. "Uchunguzi wetu
unaendelea."
"Sisi hatutangazi, lakini kazi inaendelea.
“Kuna operesheni nyingi sana zinaendelea kwa sasa na zipo katika hatua
tofauti tofauti za uchunguzi. Pia biashara hii ina uhusiano wa moja kwa
moja na utakatishaji fedha.”
Awali, akizungumza mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Kamishna Sianga
alisema mapambano yanafanyika kwa njia kuu tatu ambazo ni kuzuia
uingizwaji wake, kutoa elimu ili wananchi wakatae kutumia dawa hizo na
kama imeshindikana, kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya kwa
kuwapatia matibabu.
“Kuna wengine wametajwa kwenye orodha ni wagonjwa (watumiaji wa dawa),
hatuwakamati ili tuwafunge maana tukifanya hivyo tutajaza magereza na
haitasaidia," alisema Sianga.
"Tunawahoji watuonyeshe wanaowauzia ili kupata waingizaji na wao tunawapeleka kwenye tiba.”
Alisema jamii ya kimataifa ambayo nchi inajifunza huko, inaeleza kuwa
watumiaji wa dawa za kulevya wanatazamwa kama wagonjwa wanaohitaji
matibabu na msaada mkubwa, hivyo pamoja na kuwakamata wanapelekwa kwenye
vituo vya kutibu watumiaji wa dawa vya Hospitali ya Rufani ya Temeke,
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Rufani ya Mwananyamala,
zote za Dar es Salaam.
“Ripoti imesisitiza kuwa tuwatazame kama wenye kuhitaji msaada zaidi
kuliko kuwatazama kama watu wa kukamata na kufunga," alisema.
"Wapo wengi mtaani na hata ukiwakamata na kuwajaza kwenye magereza haitasaidia bali tutawatibu.”
HATUA MADHUBUTI
Awali, Mwakilishi Mkazi wa UN, Alvaro Rodriguez, aliipongeza serikali
kwa hatua madhubuti za kupambana na kuzuia dawa za kulevya nchini na
kwamba jitihada hizo zimeleta mwamko kwenye jamii juu ya athari za dawa
hizo.
“UN imejidhatiti katika mapambano haya. Ofisi yetu ya Makosa ya Jinai na
Dawa za Kulevya (UNODC) na Mshirika ya Umoja huo wako mstari wa mbele
kukabiliana na changamoto hii kwa kuwa na mfuko na programu ambao
zimesaidia kupunguza umaskini na kusisitiza maendeleo endelevu,”
alifafanua.
Rodriguez alisema mapambano ya dawa za kulevya yanazitaka nchi zote
kuungana kutokana na ukweli kuwa upo uhusiano wa karibu wa makosa ya
jinai, matokeo ya dawa ambayo yanahitaji huduma za afya na rushwa.
Alitaja changamoto zilizopo kuwa ni tamaduni na sheria tofauti za
kupambana na dawa hizo huku akitolea mfano wa nchi jirani ya Kenya
ambako matumizi ya mirungi yameruhusiwa wakati hapa yamekatazwa.
Mwakilishi huyo alisema Mkutano Mkuu wa 30 wa dunia katika kupambana na
dawa za kulevya, ulitoa chapisho likionyesha maamuzi ya pamoja katika
kupambana na dawa za kulevya, usafirishaji, matibabu na mambo yahusuyo
matumizi mabaya ya kemikali za viwanda kuzalisha dawa za kulevya.
Alisema ripoti ya mwaka juzi ilieleza jinsi usafiri wa majini unatumika
kufanikisha biashara hiyo, na kupongeza jitihada za nchi za ukanda wa
Afrika Mashariki kwenye Pwani na mji wa Mombasa Kenya, kufanikiwa
kupambana na uhalifu huo.
Mwezi uliopita, akiwaapisha Kamishna Sianga, Rais Magufuli alipigilia
msumari wa mwisho katika mapambano hayo kwa kueleza kuwa vita hiyo
itaendeshwa na serikali kwa mujibu wa sheria na kwamba Watanzania 1,007
wanaoshikiliwa kwenye magereza mbalimbali duniani, kwa mashtaka ya dawa
za kulevya na wafungwa 68 waliohukumiwa kifo nchini China, serikali
haitahusika kuwatetea.
Aidha, Rais Magufuli alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutomuogopa
mtu yeyote katika vita hiyo na hata ikiwa ni mkewe, Janet Magufuli,
akamatwe bila ya kujali jina.
No comments:
Post a Comment