SHABIKI
wa Yanga ambaye anaweza kuwa maarufu zaidi kwa kipindi hiki basi ni
yule Kanjunju John ambaye alimwaga machozi baada ya kikosi cha Yanga
kuchapwa mabao 2-1 na watani wao, Simba.
Kikubwa
kilichokuwa kinamliza Kanjunju ni kupoteza fedha zake Sh 50,000 ambazo
‘alibeti’ akiwa na imani kubwa kuwa timu anayoishabikia ya Yanga
inaitandika bila hofu hata kidogo.
Wakati
mechi inaanza, mambo yalionekana kwenda poa sana kwa Kanjunju, maana
Yanga iliongoza kwa bao la penalti la dakika ya tano tu mfungaji akiwa
ni Simon Happygod Msuva.
Lakini
dakika ya 66, furaha ya Kanjunju ilianza kuota mbawa, ilikuwa ni baada
ya Laudit Mavugo kusawazisha kwa kichwa akiunganisha krosi ya Shiza
Kichuya.
Kumbe
Kanjunju alizimia baada ya bao la Mavugo, akachukuliwa kwenda kupatiwa
huduma ya kwanza. Alipozinduka tayari mechi ilikuwa imefikia mwisho
dakika 90 zimeisha na hakufanikiwa kuliona bao la pili la Kichuya.
Alipouliza
matokeo, watu hawakuwa na hiyana, walimueleza ukweli Kanjunju kwamba
Simba wameshinda 2-1 na Kichuya ndiye aliyefunga bao la pili. Safari hii
Kanjunju akawa imara maana hakuzimia, akaanza kumwaga machozi na ndiyo
alihojiwa na waandishi na kujulikana kwa mashabiki wengine.
Kanjunju
ni shabiki wa soka kama wengine lakini ana mambo kadha wa kadha unaweza
ukajifunza kupita yeye na mwisho machozi yake yakawa ni sehemu ya
salamu kuwakumbusha mambo kadhaa viongozi wa soka bila ya kujali ni wa
klabu gani au shirikisho.
Kanjunju
huyu, anaweza kuonekana kama ni mtu asiye na fikra sahihi. Vipi mtaji
wake wa biashara anaamua ‘kubeti’ akiwaamini Yanga? Ni kitu
kinachoshangaza lakini lazima viongozi wajue kupitia machozi ya Kanjunju
kuna watu wana mapenzi makubwa na timu zao.
Kanjunju
anaiamini sana Yanga, kuamini kwake haiwezi kuwa anamuamini Mwenyekiti
Yusuf Manji pekee. Badala yake analiamini benchi la ufundi pia wachezaji
ambao ndiyo wanaocheza uwanjani.
Imani
ya mashabiki kwenu viongozi, makocha na wachezaji ni kubwa sana. Mtu
anayewekeza mtaji wake kwa imani kwenu maana yake anawaamini sana na
anawachukulia kama watu wanaothamini wanachokitumikia.
Maana
yake mliopata nafasi ya kuitumikia Yanga au klabu nyingine iwe Simba na
kadhalika, hakika mnapaswa kuijua thamani hiyo kuwa mmebeba mioyo ya
kina Kanjunju wengi wakiwemo wale wanaopoteza maisha yao.
Wanawekeza
uhakika wa maisha yao, yaani mtaji kwa kuwa wanawaamini. Je, wachezaji
au makocha wanajua kuna watu wako tayari kwa hilo kutokana na
wanavyowaamini? Kanjunju anaiamini Yanga akijua ina watu sahihi na
wanaofanya kazi kwa weledi, mapenzi na juhudi kubwa. Je, ni kweli
mliopata nafasi hiyo mnaitumikia hivyo?
Kanjunju
alizimia, si jambo la mzaha. Lakini mtu mzima alimwaga machozi mbele ya
hadhara bila ya woga. Vizuri kila anayeguswa na hili hasa kwa
wachezaji, makocha na viongozi wajue hizi klabu zenye mashabiki wengi,
zinaumiza mioyo na hisia za watu.
Kufungwa
ni lazima, lakini ukifungwa huku unaonekana ulikuwa unapigana. Hakuna
atakayekulaumu. Hali ya kujituma au juhudi za wazi zisiwe kwenye Yanga
au Simba pekee, kila mwenye sehemu yake ya kazi lazima afanye juhudi
akijua kuna sehemu watu wanamuamini.
Tokea
zaidi ya miaka 17 niliyoanza uandishi wa habari, sijapunguza juhudi,
ubunifu na sijawahi kuchoka kwa kuwa najua nina watu wanaoniamini na
sipendi kuwaangusha hata kama mimi ni binadamu, si mkamilifu.
Si
vizuri kama alivyofanya Kanjunju ‘kubeti’ mtaji wake. Lakini ni vizuri
kuwaamini watu wako ukiamini katika soka kufungwa kupo. Lakini narudia
kusisitiza, wanaopata nafasi wakijua nyuma yao kuna watu, wayathamini
mapenzi yao na hii iwafikie hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
kwamba watu wanaupenda mpira na wanaumia sana hivyo, utendaji wao
usijali ubinafsi zaidi na hasa kwa ajili yao. Iwe kwa ajili ya
Watanzania, maana kina Kanjunju wako wengi.
No comments:
Post a Comment