Kwa siku tatu mfululizo, mjadala mkubwa umekuwa ni jina la mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Aliingia studio za Clouds TV Ijumaa usiku akiwa na askari waliokuwa na
silaha za moto, akajadiliwa katika mitandao ya kijamii kutokana na
kitendo hicho, Jumapili akawa sehemu ya mahubiri ndani ya Kanisa la
Uzima na Ufufuo, lakini jana Rais John Magufuli akamhakikishia kibarua
chake, jambo lililoongeza kasi ya mjadala.
“Makonda Amtega Rais Magufuli”, “Makonda Katika Moto kwa Kuvamia Clouds
Usiku”, Makonda, Gwajima Waanza Vita Upya”, na “Makonda ‘Ateka’ Clouds
Media” ni baadhi ya vichwa vya habari vya magazeti ya jana kuonyesha
kitendo cha mkuu huyo wa mkoa kilivyotikisa nchi.
Habari hizo zote zinazungumzia kitendo cha Makonda kuingia studio za
Clouds TV inayomilikiwa na Clouds Media Ijumaa usiku, akiwa na askari
waliovalia sare na kiraia na ambao walishika silaha za moto na kukariri
wadau wakitaka Rais amchukulie hatua.
Na jana asubuhi wadau wa habari, Waziri Nape Nnauye, mwenyekiti wa Chama
cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat), Jukwaa la Wahariri (TEF),
wahariri, wasanii na vyombo vingine vya habari vilikuwa vikitoa pole kwa
uongozi wa Clouds na kulaani kitendo hicho cha Makonda.
Huku wananchi wakiendelea kupaza sauti kutaka atengue uteuzi wa mkuu
huyo, Rais Magufuli alitumia ufunguzi wa mradi wa ujenzi wa barabara za
juu za kupishana magari katika makutano ya Barabara ya Sam Nujoma na
Morogoro kueleza ya moyoni kuhusu mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.
Rais alizungumzia taarifa zinazoendelea kujadiliwa mitandaoni kuwa hazina tija na kumtaka “Makonda aendelee kuchapa kazi”.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkubwa mtandaoni kuhusu
Makonda na utata wa elimu yake, utajiri wa ghafla na tukio la Ijumaa
usiku. Ilikuwa ni takriban saa tatu baada ya mkurugenzi wa vipindi na
uendeshaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba kuzungumza kuhusu tukio hilo
katika kipindi cha televisheni cha 360, ambacho Rais Magufuli ameshapiga
simu mara tatu kueleza jinsi anavyokifuatilia.
Ruge alikuwa akithibitisha habari zilizoenea mitandaoni tangu Jumamosi
kuwa Makonda alifika studio za Clouds TV Ijumaa usiku, akiwa ameambatana
na askari wenye silaha za moto na kuchukua kwa nguvu sehemu ya kipindi
cha Shilawadu kilichokuwa kimezuiwa kurushwa kutokana na kutokidhi
matakwa ya kitaaluma.
Shilawadu ni kifupisho cha Shirikisho la Wambea Duniani na ni kipindi
ambacho kinazungumzia tuhuma za watu mbalimbali maarufu na katika
mahojiano ya 360, Ruge alisema alihisi habari ambayo aliizuia isitoke
hadi itakapokidhi vigezo vya kitaaluma, ilikuwa ina uhusiano na Makonda
baada ya kuambiwa na mmoja wa watangazaji wa Shilawadu kuwa inamuhusu
mwanamke ambaye anadai amezaa na Askofu Josephat Gwajima, mpinzani
mkubwa wa mkuu huyo wa mkoa.
Taarifa kuhusu Makonda kuhusika katika sakata hilo zilipamba moto
Jumapili asubuhi na zikafuatiwa na video zinazomuonyesha mkuu huyo wa
mkoa akiingia ofisi hizo akiwa na askari wenye silaha.
Kusambaa kwa video hizo kuliibua mjadala mkubwa kutokana na wengi kuhoji
sababu za Rais Magufuli kutochukua hatua haraka kama alivyofanya kwa
watumishi wengine wa umma, akiwemo Charles Kitwanga aliyekuwa Waziri wa
Mambo ya Ndani baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa.
Kutokana na maswali mbalimbali kuibuka, huku Clouds ikitakiwa ieleze
ukweli, Ruge alilazimika kueleza kilichotokea, akitumia kipindi cha
televisheni ya Clouds TV cha 360 kinachorushwa kila siku asubuhi.
“Paul (Makonda) ni rafiki yetu, lakini ametukosea, huwezi kuja ofisini
kwetu ukiwa na mabunduki tena usiku,” alisema Ruge ambaye vituo vyake
vya redio na televisheni vimekuwa vikirusha moja kwa moja shughuli za
Makonda.
“Sijutii urafiki wetu na mkuu wa mkoa, bali nalaumu vitendo vyake na
anapokosea lazima aambiwe ukweli kuwa kakosea. Makonda ni rafiki yetu,
lakini mimi urafiki na bunduki siutaki kabisa. Urafiki wa wali na
maharage freshi.”
Ruge, ambaye usoni alionekana kuwa asiyetaka masihara, alisema hakutaka
kumtafuta Makonda baada ya tukio hilo kwa kuwa mkuu huyo wa mkoa ndiye
aliyewakosea.
“Nataka nirudie kwamba urafiki unatengeneza mazingira ya kwamba, ok. Hii
unataka kuifanya vizuri zaidi, kitengenezee mazingira mazuri zaidi.
Tutakuruhusu ufanye, sio hapa atafanya hata kule kama ambavyo tunaruhusu
watu wengine pia wafanye,” alisema Ruge.
“Mimi kwa kweli nampongeza upande mmoja; ni mtu ambaye kwa kweli amekuwa
akitumia nafasi vizuri, kwa sababu sio kosa kusema kwamba mimi nina
hiki, naomba niki-edit vizuri mnisaidie kukirusha, sio kosa. Kosa ni
pale ambapo unapotaka kupanda watu kichwani.
“Kosa ni pale ambapo unapotumia nafasi yako kwa ubaya.”
Ruge alisema yeye anasimamia chombo kilicho na watu zaidi ya 200 na
ambao ni vijana wadogo, kulinganisha na Makonda ambaye anasimamia watu
milioni tano.
“Kwa bahati mbaya wale mia mbili wananitazama kama mtu ambaye ni mfano.
Nisipowatetea wao, huyu atakuja leo. Akija kila siku kiongozi mwingine?”
alihoji Ruge.
“Tubadilishe mtazamo wetu sasa maana viongozi wanashindana na wasanii
kutafuta kiki kwenye mitandao ya kijamii. Viongozi wetu wanapenda
kumzungumzia Mwenyezi Mungu, lakini hawajui kuwa dhambi za binadamu
zinaumiza zaidi kuliko kumuudhi Mungu.”
Msimamo wa Magufuli
Hata hivyo, Rais John Magufuli alimtaka Makonda kuendelea kuchapa kazi na kwamba yeye hafanyii kazi maneno ya kwenye mitandao.
Magufuli, ambaye wakati mwingi wa hotuba yake alionekana akisoma,
alionekana kuanza kutotegemea alichokiandaa alipoanza kuzungumzia suala
la Makonda.
Alisema kuna baadhi ya watu wanaingilia majukumu yake wakati yeye ndiye
mwenye uamuzi na kwamba hapangiwi kazi ya kufanya kwa sababu anajiamini.
“Tunaendekeza mambo ya udaku wakati hayatusaidii kupata chakula,
kupunguza foleni Dar es Salaam, kupeleka watoto shule, kupata maji ya
kunywa, kupata maendeleo. Tuzungumze uchumi na maendeleo ya wana-Dar es
Salaam,” alisema Rais Magufuli.
“Mnahangaika kupost (kutuma) mara hili, mara lile, mpaka watu wengine
wananiingilia nifanye mambo wanayotaka. Ukinipangia ndiyo unapoteza.
Mimi ni Rais ninayejiamini.”
Kwa wiki takriban tatu, kumekuwa na habari katika mitandao zikimuhusisha
Makonda na mtu anayeitwa Daudi Bashite aliyesoma Shule ya Msingi
Koromije na Sekondari ya Pamba na kumaliza kidato cha nne kwa kupata
daraja la sifuri.
Mmoja kati ya watu wanaoongoza kushamirisha habari hizo ni Askofu
Gwajima, ambaye amesema anamfahamu na anao ushahidi wa vyeti na watu
waliosoma na Bashite na hivyo kumtaka Makonda athibitishe utambulisho
wake, la sivyo ataweka bayana kila kitu.
Lakini Rais Magufuli, ambaye Serikali yake imekuwa ikifanya uhakiki wa
wafanyakazi wa umma na elimu yao, alisema habari za mitandaoni hazina
tija kwake na kuwataka wakazi wa Dar es Salaam kuchapa kazi kwa ajili ya
maendeleo badala ya kupoteza muda kufuatilia udaku kwenye mitandao.
Alisema hawezi kupangiwa nini cha kufanya.
“Najua mwenyewe nani anatakiwa kuwa wapi, akae wapi, ni mimi ninayepanga. Ninajua wamenielewa,” alisema Rais.
“Kwa hiyo Makonda wewe chapa kazi. Nasema chapa kazi. Suala la kuandikwa
kwenye mitandao sio tija kwangu. Hata mimi ninaandikwa kwenye mitandao,
kwa hiyo nijiuzulu urais? Chapa kazi,” alisema Rais akimuangalia
Makonda, ambaye alisimama na kuinamisha kichwa kuonyesha kukubali.
“Kwa hiyo niwaombe ndugu zangu Watanzania, tunapoteza muda mwingi kwa
mambo yasiyo ya msingi. Tuwatumikie Watanzania. Watanzania wana shida
nyingi za kufanya. Wanahitaji maji, wanahitaji barabara, wanahitaji
elimu, wanafunzi wa chuo kikuu wanahitaji wapate mikopo, Ni mambo yote.
wanahitaji afya nzuri. Hilo ndilo jukumu letu sisi viongozi.
“Kwa hiyo niwaombe Watanzania wenzangu wa vyama vyote, tusijisumbue na mambo yasiyo na msingi.”
Ruge asimulia
Kabla ya kutoa hotuba hiyo, Ruge alieleza mkasa wote ulivyokuwa tangu
Alhamisi wakati Makonda alipoenda makao makuu ya Clouds na kuongea na
watangazaji wa kipindi cha Shilawadu.
Ruge alisema siku hiyo walikuwa na kikao na watu wa TCRA na baada ya
hapo alitoka nje ambako alimkuta Makonda akiwa pamoja na vijana
wanaofanya kipindi cha Shilawadu na alipowauliza kuwa ni kwema alijibiwa
kuwa walikuwa katika mazungumzo ya kawaida tu.
“Nikiwa kwenye gari nikijiandaa kutoka, kijana mmoja wa Shilawadu
alinifuata na kuniambia kuna mahojiano amefanya na mtu anaedai amezaa na
Gwajima nikamuuliza kwa hiyo,” alisema Ruge.
Alisema kijana huyo alimwambia kuwa wameshindwa kumpata Gwajima na hivyo
akawaambia wasirushe hicho kipindi hadi wampate askofu huyo.
Na kwa kuweka msisitizo, Ruge alimwambia meneja wa vipindi anayeitwa
Kerry kuwa kama Askofu Gwajima hajapatikana, kipindi hicho kisirushwe na
baadaye kumpigia simu ofisa rasilimali watu kumweleza suala hilo.
Pia, Ruge aliwaambia waandaaji wa kipindi hicho wamueleze hata Makonda
kuwa hawangeweza kukirusha kutokana na upande wa pili kutopatikana.
“Tena nikamwambia Kerry kwa masihara kuwa ikiwezekana ayapoteze kabisa
hayo ‘material’ kwa sababu hata Shilawadu wenyewe walikuwa wanavutana
juu ya habari hiyo,” alisema Ruge.
Ruge aliendelea kuwa siku hiyo hiyo saa 10:00 jioni alipigiwa simu na
Askofu Gwajima akimueleza kuwepo kwa habari inayomuhusu, lakini
akamhakikishia kuwa habari hiyo haipo na haitaruka kwa sababu haijakidhi
vigezo.
Mkurugenzi huyo alisema jambo la kushangaza majira ya saa 4:45 usiku
Ijumaa alipokea simu kutoka kwa ofisa rasilimali watu akimueleza kuwa
mkuu wa mkoa ameingia ofisini akiwa na askari sita wenye silaha.
Alisema baada ya simu hiyo ilifuatia simu ya mkurugenzi mtendaji wa
kampuni hiyo, Joseph Kusaga akimueleza kuwa analaumiwa na Makonda kuwa
amezuia kipindi chake.
Mtangazaji mualikwa wa 360, Masoud Kipanya aliuliza kama Makonda huwa
ana vipindi vyake Clouds, lakini Ruge alisema hakuna kitu kama hicho.
Alisema baadaye Kusaga alitaka wafanye mazungumzo na Makonda kuhusu suala hilo.
“Mimi nikamwambia siwezi kwenda kwa sababu hata mkuu wa mkoa hajaonyesha
heshima kwa sababu anao uwezo wa kunipigia simu muda wowote. Kwa nini
hajafanya hivyo mpaka avamie,” alisema Ruge.
Ruge alisema baadaye alimpigia simu Makonda na akamuuliza sababu za
kwenda ofisi za Clouds na watu wenye bunduki, lakini Makonda akamjibu
kuwa amefanya hivyo kwa sababu amezuia kipindi chake.
“Kwanza sio kipindi chako (Makonda). Mimi ndiye mkurugenzi wa vipindi,
na hivi vipindi viko chini yangu,” alisema Ruge akikumbuka mazungumzo
yake na Makonda kwenye simu.
Ruge alisema Makonda alimuelezea kuhusu kipindi kinachomuhusu mwanamke
anayedai amezaa na Askofu Gwajima, lakini akamjibu kuwa upande wa pili
haujapatikana na kumueleza umuhimu wa kusimamia weledi kwa kila mtu
kupewa nafasi.
Alisema Clouds kama chombo cha habari wameumia kuona tukio hilo
linafanywa na rafiki yao ambaye angeweza kuhoji kwa namna nzuri lakini
sasa amesababisha vijana wa Shilawadu kutokuwa sawa mpaka wamefikia
hatua ya kuomba likizo ili watulize akili zao kwa kuwa tayari
washaingiwa uoga.
“Tubadilishe mtazamo wetu sasa maana viongozi wanashindana na wasanii
kutafuta kiki kwenye mitandao ya kijamii. Viongozi wetu wanapenda
kumzungumzia Mwenyezi Mungu lakini hawajui kuwa dhambi za binadamu
zinaumiza zaidi kuliko kumuudhi Mungu,” alisema Ruge.
Alisema video zinazosambaa katika mitandao ya kijamii likihusisha tukio
lile ni za kweli, lakini hajui ni nani aliyezitoa kwa sababu pale kuna
CCTV kamera na kila mfanyakazi anajua wapi zinafanyia kazi.
Pia alizungumzia habari zilizosambaa kuwa alishikiliwa na polisi Jumapili.
“Watu walisema eti niliwekwa ndani polisi lakini sio kweli nilienda tu
kuripoti kwa ajili ya taarifa maana linapotokea jambo lolote linalohusu
uvamizi wa silaha ni lazima maelezo yachukuliwe ili kuepusha
upotoshaji,” alisema Ruge.
Pia, Ruge alisifu vyombo vya habari kwa kumuonyesha mshikamano, akisifu
hata wapinzani wao wakubwa kwamba wamesikitishwa na tukio hilo na kuomba
wadau wote wa habari kusimama pamoja katika hilo kuhoji haki na heshima
ya vyombo vya habari.
Nape awatembelea
Katika tukio jingine, hata kabla ya Rais Magufuli kuonyesha kumuunga
mkono Makonda, Waziri Nape alifika ofisi za Clouds Media zilizopo
Mikocheni saa 3:25 asubuhi, akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Idara ya
Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbas pamoja na mwenyekiti wa Moat, Reginald
Mengi.
Akiwa katika kituo hicho, Nape alisema Serikali inalaani kitendo
kilichotokea katika nchi ambayo imesaini mikataba ya kimataifa ya
kulinda uhuru wa habari na kwamba sheria zipo na zinapaswa kufuatwa
“Tumeunda timu ya watu watano kufanya kazi kwa saa 24 ili wapate maelezo
ya RC baada ya hapo tutaeleza hatua tutakazozichukua kama Serikali.
Lakini kabla ya kuchukua hatua zozote, tunataka kusikia kutoka kwa mkuu
huyo,” alisema Nape.
Waziri Nape alikifananisha kitendo hicho kama mapinduzi ya kijeshi na
kusema anaanza kuona dalili za wanasiasa kukosa ngozi ngumu.
“Kwakweli inatisha, haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu. Hii
inatokea tu kwenye nchi zenye mapinduzi ambako wanaopindua huvamia redio
na kujitangaza,” alisema Nape.
Alisema huwezi kuzungumzia suala la ulinzi mdogo kuwepo Clouds kwa
sababu unaweza ukawepo hata wa polisi, lakini akishakuwepo mkuu wa mkoa
hawana cha kufanya.
“Nimeteua kamati ndogo inayoongozwa na mkurugenzi wa habari. Nimewaagiza
wamhoji leo (jana) mkuu wa mkoa ili tupate nini kiliwasukuma wafanye
walichofanya, halafu kesho (leo) mchana tutakuwa na press conference
(mkutano na waandishi) kueleza hatua tutakazochukua,” alisema Nape.
Mengi azungumza
Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa Moat alisema wako pamoja na
Clouds na watashirikiana kupambana na unyanyasaji kwa vyombo vya habari
na kuwataka waandishi kuendelea kufanya kazi bila woga.
Alisema sura moja ya mwandishi wa habari ni kutokuwa mwoga hivyo jambo lililotokea lisiwatie hofu.
“Jambo lililofanyika ni la hatari sana. Na lazima tujiulize mtu huyu
(Makonda) anapata wapi ujasiri huu?. Kama alikuja na bunduki hapa
anaweza kwenda nazo popote na pengine kuna siku atazitumia,” alisema
Mengi.
Alisema ana imani kuwa Rais Magufuli na waziri wa habari wana upendo kwa
vyombo vya habari lakini mapenzi hayo lazima yaonyeshwe kwa vitendo.
Kamati ya Bunge yatinga Clouds
Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ilitembelea
ofisi za Clouds Media na mwenyekiti wake, Peter Serukamba alisema
wametumwa na Spika wa Bunge.
“Alichofanya mkuu wa mkoa kwa namna yoyote ni matumizi mabaya ya
madaraka. Sisi kama kamati tunasubiri Serikali wameunda kamati na sisi
tutashauri baada ya kupata maoni ya hiyo kamati,” alisema Serukamba.
Huku akisisitiza haja ya waandishi wa habari kulindwa wanapotimiza
majukumu yao, Serukamba alisema viongozi wa Serikali hawapaswi kutumia
vyombo vya ulinzi na usalama kufanya lolote wanalotaka kinyume cha
sheria.
“Leo (jana) amekuja kwenye vyombo vya habari, kesho atakwenda kwenye
restaurant, keshokutwa atakwenda kwenye nyumba zetu. Niviombe sana
vyombo vya usalama, fanyeni kazi kulingana na sheria zilizowaweka
madarakani. Nchi inaendeshwa na sheria,” alisema Serukamba.
Alisema jambo hilo ni gumu kulifikiria na ni dalili za ulevi wa madaraka.
“Nilikuwa najiuliza, wakipanda hapa na mabunduki ingetokea bahati mbaya
bunduki ile kukatokea lolote, risasi ikafyatuka akafa mtu, leo
tungeongea nini? Huku ndiyo kuchapa kazi?” alihoji.
“Lakini kwa vyovyote vile kilichofanyika hakikubaliki kwa jamii ya
Watanzania. Kutoka miaka 50 ya uhuru, hakuna mkuu wa mkoa amewahi
kufanya haya. Tumepitisha sheria ile ya habari, lakini na waandishi wa
habari walindwe,” alisema.
Hata hivyo, Serukamba aliwataka waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari kuepuka kutumiwa na wanasiasa kwa masilahi yao.
“Jambo hili ni fundisho kwa waandishi wa habari. Msikubali kutumiwa na
sisi wanasiasa. Inawezekana matokeo ya jambo hili ni kwa sababu sisi
wanasiasa tunakuja kwenye vyombo vya habari, tunatengeneza ujamaa na
tunaweza kulazimisha mambo ambayo ni nje ya utaratibu,” alisema
Serukamba.
Sugu alaani
Akizungumzia tukio hilo, Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Joseph Mbilinyi alisema walioguswa si Clouds Media peke bali
tasnia nzima ya habari.
“Kwa kweli kitendo kilichotokea ni cha kulaaniwa. Hii siyo Tanzania
tuliyokuwa tukiitarajia na ndiyo maana tuko hapa kunyoosha mambo kama
viongozi. Shambulio lililofanywa jana (juzi) si kwa Clouds peke yake,
bali ni kwa industry nzima,” alisema Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alimtaka Makonda kuomba radhi kwa jambo alilofanya ili kulinda uadilifu wake.
“Makonda kama kijana anafanya makosa ya kimkakati yanayomharibia sifa
kila kukicha. Naamini kiustaarabu si dhambi ukikosea ukaja hadharani
kuwaomba radhi Clouds. Ana wajibu wa kuja kuomba radhi kwa kitendo cha
kuingia na askari wakiwa na silaha na kutengeneza taharuki hii,” alisema
Bashe.
UTPC kuchukua hatua
Nao Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC) umeonya kuwa unaweza
kumchukulia hatua Makonda, ikiwemo kumtenga katika kazi zake iwapo
mamlaka yake ya nidhamu haitamchukulia hatua.
Rais wa UTPC, Deogratias Nsokolo alisema kitendo cha kiongozi wa
Serikali kuvamia ofisi akiambatana na askari wenye silaha ni cha jinai
na hakijawahi kutokea nchini.
“Mtu yeyote anayetaka kulazimisha habari gani itoke au isitoke anafinya
uhuru wa habari kwani kazi ya uandishi wa habari ina miiko yake hiyo na
inayotumika kuamua ni habari gani itumie au isitumike,” alisema Nsokolo.
Mkurugenzi wa UTPC, Abubakar Karsan alisema hivi karibuni Serikali
imepitisha sheria inayoitwa uhuru wa habari na moja kati ya vipengele
katika sheria hiyo inawapa mamlaka Serikali kuchagua habari gani itoke
au isitoke, kwa maana hiyo kitendo cha mkuu wa mkoa kuvamia kituo hicho
cha habari swali la kujiuliza je, sheria hiyo imeanza kutekelezeka?
TLS watoa kauli
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amemshauri
Rais Magufuli atengue uteuzi wa Makonda haraka iwezekanavyo kabla
hajachafua zaidi taswira ya Serikali yake.
Pia amemshauri Rais Magufuli kumchukulia hatua stahiki kamanda au mkuu
wa kikosi chochote cha jeshi lolote aliyeruhusu askari wake kutumiwa na
Makonda kwa namna iliyoripotiwa.
Katika taarifa yake kwa umma, Lissu amesema Makonda hastahili kuendelea kwenye madaraka hayo kwa siku moja zaidi.
No comments:
Post a Comment