Kada wa Chadema katika Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, Anitha Swai ameuawa katika tukio lililogubikwa na wingu zito.
Taarifa
za awali zilizopatikana usiku wa kuamkia leo zimedai kuwa Anitha
ambaye aligombea ubunge wa viti maalum mwaka 2015, alitekwa nyara
wilayani Rombo na kuuawa maeneo ya TPC nje kidogo ya mji wa Moshi.
Vyanzo
mbalimbali vya habari vimedokeza kuwa mara ya mwisho mwanasiasa huyo
alionekana akiwa na watu wawili wilayani Rombo siku ya Jumatatu,
Februari 27 na kuaga wanaelekea Arusha.
Hata
hivyo, tangu siku hiyo Anitha hakuonekana hadi maiti yake
ilipogunduliwa jana (Alhamisi) jioni maeneo ya TPC huku gari lake likiwa
limetelekezwa maeneo ya Bomambuzi mjini Moshi.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha
kuokotwa kwa mwili huo, lakini amekataa kuthibitisha kama ni wa kada
huyo wa Chadema.
"Ni
kweli kuna tukio hilo, lakini ninachoweza kusema bado hajatambuliwa na
mwili wake umepelekwa KCMC ili ndugu waweze kuutambua," amesema.
Hata
hivyo, Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Mawenzi mjini Moshi, Hawa
Mushi amethibitisha kuwa aliyeuawa ni kada wa chama chao, lakini chanzo
na nani waliohusika hakijajulikana.
Hawa
amesema taarifa zilizothibitishwa ni kuwa mwili wake ulipatikana maeneo
ya TPC huku simu iliyopatikana katika gari yake ndiyo iliyosaidia
kumtambua.
No comments:
Post a Comment