Mwezi wa tatu maarufu kama Machi ulioanza leo, umegubikwa na matukio
matano ambayo Watanzania kutoka pande zote za nchi wanatarajiwa
kuyashuhudia.
Tayari Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kilishazungumza takriban mwezi
mzima uliopita juu ya kusudio la kutangaza mgogoro na Serikali unaolenga
kudai haki ya madai ya wanachama wake.
CWT imekuwa ikilalamika kwa muda sasa juu ya madai mbalimbali ya walimu, yakiwamo yanayohusiana na mishahara na malipo mengine.
Rais wa chama hicho, Gratian Mkoba anasema madai ya walimu yanafikia
takriban Sh800 bilioni na awali waliitaka Serikali iwe imeyalipa ifikapo
Februari 28, vinginevyo wataanza mgogoro huo leo.
Katika kukoleza chumvi kwenye kidonda, Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi
Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya alisema jana kwamba, wanaunga mkono
hatua zozote zitakazochukuliwa na CWT kwa lengo la kuishinikiza
Serikali kuwalipa madai yao.
“Tunawanga mkono CWT waendelee na mchakato wao kwa sababu Serikali
haitaki kutoa kauli zenye kuwaletea matumaini walimu,” alisema.
Mbali ya sakata hilo, suala lingine linalokusudiwa kuutikisa mwezi huu
nchini ni mfumo wa kubadili mtandao wa simu bila ya kubadili kadi (MNP).
Mfumo huo unawapa uhuru wateja wa mitandao yote ya simu nchini kuhama
kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine wakati wowote wanaoona unafaa.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa
atazindua rasmi mfumo huo leo katika ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba alisema lengo ni kuwapa
uhuru wateja kutumia mtandao bora zaidi na kuongeza ushindani kwa
kampuni ili kuboresha huduma zao.
“Uanzishwaji wa MNP ni kwa mujibu wa kanuni za mwaka 2011. Kanuni hizi
zinawataka watoa huduma za simu za kiganjani kuwezesha huduma hii katika
mitandao yao,” alisema Kilaba.
Mbali na mambo hayo mawili, lingine la tatu ni lile la waumini wa
madhehebu ya Kikristo nchini na duniani kote kuanza mwezi wa kujinyima
kukumbuka mateso ya Yesu Kristo kwa kufunga kula, maarufu kama kipindi
cha Kwaresma.
Wakristo duniani kote kuanzi leo watasali katika Jumatano ya Majivu, misa ambayo ni ufunguzi rasmi wa kipindi cha Kwaresma.
Ibada ya Majivu huhusisha waumini kupaka majivu ikiwa ni ishara ya
mwanzo wa kuanza mfungo wa siku 40 wa kukumbuka mateso ya Yesu Kristo.
Jambo lingine ni lile la marufuku ya viroba ambalo zuio lake linaaza leo.
Iwapo utekelezaji wake utakuwa na ufanisi utasaidia kuzuiliwa kwa pombe
hizo kali zinazowekwa kwenye pakiti za plastiki, maarufu kama viroba.
Utekelezwa wa marufuku hiyo ya Serikali unaanza huku kukiwa na uwezekano
wa wadau wa biashara hiyo kufungua kesi kupinga utekelezwa wa agizo
hilo lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Sakata hilo lilianza Februari 20 wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Rais anayeshughulikia Mazingira, January Makamba alipotangaza
marufuku hiyo huku akiwataka watengenzaji wa pombe hizo watafute
utaratibu ulioandaliwa na Serikali wa kutumia chupa badala ya mifuko
midogo ya plastiki.
January aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba, operesheni ya
kukagua utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe ya viroba itaendeshwa
na kamati za ulinzi na usalama na kamati za mazingira za ngazi zote
kuanzia mkoa hadi mtaa ambazo zitawajibika kuwasilisha taarifa za
operesheni hiyo Tamisemi.
“Ukikutwa unakunywa, unauza na utengeneza au kuingiza viroba
utachukuliwa hatua kali zikiwamo faini na kifungo au vyote kwenda
sambamba,” alisema waziri huyo.
Mwezi huu pia unaanza huku awamu ya kwanza ya taasisi za Serikali
kuhamia na kuanza rasmi shughuli zake mjini Dodoma baada ya kazi ya
uhamaji kumalizika jana.
Agizo la kuhamia Dodoma lilitolewa na Rais John Magufuli mwaka jana
kuwa, kabla ya kumaliza miaka mitano ya awamu ya kwanza ya utawala wake,
Serikali itakuwa imehamia Dodoma.
Baada ya tangazo hilo la Rais Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
aliitikia wito huo wakati wa sherehe za maadhimisho ya kumbukumbu ya
siku ya Mashujaa mjini Dodoma, akitaka nyumba yake ikamilike haraka.
Pia alitangaza kuwa awamu ya kwanza ya uhamaji itahusisha mawaziri na
manaibu wao, makatibu wakuu na manaibu wao na wasaidizi wao, huku ile ya
pili itaanza Julai baada ya Bunge la Bajeti. Uhamaji huo utakuwa kwa
awamu sita na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020 pale
Rais atapohamia rasmi mjini humo.
No comments:
Post a Comment