Wednesday, March 22, 2017

MAJIBU TIMU YA NAPE YASUBIRIWA


IMU iliyoundwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ya kuchunguza suala la kilichotokea Clouds Media Groups wiki iliyopita, haijakamilisha kazi yake hadi kufikia jana usiku.

Nape aliunda timu hiyo ya watu watano juzi ikiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbas, na aliipa muda wa saa 24 hadi jana iwe imekamilisha kazi yake.

Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni, timu hiyo ilikuwa haijawasilisha taarifa yake kwa waziri huyo na hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu kutowasilishwa kwa taarifa hiyo.

Lakini jana mchana, katikaakaunti yake ya Tweeter, Waziri Nape aliandika: “Kuna simu nyingi juu ya ripoti. Nawaomba tutulie Kamati wanamaliza kazi yao, ikikamilika tutaarifiwa muda na mahali nitakapokabidhiwa.”

Akizungumza Dar es Salaam juzi baada ya kutembelea Clouds Media Group, Mikocheni, Nape alisema kama serikali, kilichotokea ni kitendo ambacho kimewashtua wengi na hata dunia kwa ujumla kwa kuwa hata katika historia haijawahi kutokea suala kama hilo.

Alisema kutokana na kilichotokea, ameunda timu ya watu watano wakifanya kazi kwa saa 24 ili kujua na upande wa pili ambao ni wa Makonda unazungumziaje suala hilo na baadaye watamkabidhi ripoti ambayo ataitoa leo saa 8:00 mchana.

Aliwataja wanaounda timu hiyo itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Abbas Hassan, ni Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mabel Masasi, Mhariri Mwandamizi kutoka Kampuni ya The Guardian, Jesse Kwayu, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamhuri na Mhariri wa Wapo Radio, Neng’ida Johannes.

Waziri Nape alisema serikali imesikitishwa na jambo hilo, lakini lazima kutenda haki kwa kumsikiliza pia mkuu wa mkoa na watu wake ili kujiridhisha halafu ndipo hatua nyingine zitakapoweza kuchukuliwa.

Naye Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba alilezea namna Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alivyovamia ofisi za chombo hicho cha habari akiambatana na askari waliobeba silaha.

Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika kwenye kipindi kinachorushwa na kampuni hiyo juzi, Mutahaba alisema wanalaani kitendo hicho cha Makonda kwa kuwa kimewaacha katika hali mbaya wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Alisema chanzo cha tukio hilo, kilianza tangu Alhamisi iliyopita wakati uongozi wa kampuni hiyo ulipokuwa kwenye kikao na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRA), ambapo walipata ugeni wa RC Makonda katika kikao hicho.

“Baada ya hapo wakati kikao kimemalizika nikiwa natoka nikakutana na vijana wanatangaza katika kipindi cha Shirika la Wambea Duniani (Shilawadu) kupitia kampuni hiyo, wakiwa wanazungumza na mkuu huyo wa mkoa,” alisema Mutahaba.

Alisema mmoja wa vijana wale alimfuata na kumueleza juu ya kuwepo kwa fununu za habari kubwa inayomhusu Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kuzaa na mmoja wa waumini wake, lakini bado fununu hizo pamoja na kukamilika upande mmoja, hazijathibitishwa upande wa pili.

“Niliwaambia kuwa kama habari hiyo hata kama ni nzuri vipi kama bado haina upande wa pili kama maadili ya taaluma ya uandishi wa habari yanavyotaka kamwe isirushwe hewani. Sikuishia hapo nilimpigia simu mkuu wa vipindi Carry, nikamuonya asiruhusu habari hiyo iruke hewani kama haijawa balanced,” alifafanua.

Alisema siku hiyo, majira ya saa 10 jioni alipigiwa simu na Askofu Gwajima akiulizia taarifa za kuwepo kwa habari inayomhusu inayotarajiwa kurushwa katika vyombo vya habari vya kampuni hiyo kupitia kipindi cha Shilawadu.

Alisema alimjibu mtumishi huyo wa Mungu kuwa ni kweli alikuwa na taarifa za kuwepo kwa habari hiyo, ingawa yeye mwenyewe haifahamu kiundani na kufafanua kuwa alishaagiza isirushwe hewani mpaka itakapokamilika kwa upande wa pili kupatikana na baadaye kupata habari kwamba Makonda amevamia kituo hicho akishinikiza habari hiyo itoke.

No comments:

Post a Comment