Tuesday, March 14, 2017

LISSU, MASHA WATINGA KORTINI UCHAGUZI WA TLS

WAGOMBEA wawili wa nafasi ya Urais na mmoja wa nafasi ya Makamu wa Rais katika Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu na Lawrence Masha, wamewasilisha maombi ya kujumuishwa kama wadaiwa katika kesi ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi wa TLS.

Mwingine aliyepeleka maombi hayo katika kesi iliyofunguliwa na Wakili Godfrey Wasonga wa Dodoma, ni Godwin Ngwilimi anayewania nafasi ya Makamu wa Rais wa TLS katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii jijini Arusha.

Shauri hilo liko mbele ya Jaji Awadhi Mohammed wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma. Katika chemba ya Mahakama Kuu jana, Ngwilimi alisema ni miongoni mwa waleta maombi ya kuunganishwa katika shauri hilo.

Kwa upande wake, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema “nina maombi ya kuunganishwa kwenye shauri hili, tumeomba mimi na Lawrence Masha, kwani tuna mashaka makubwa na kanuni zilizotumika.” Hata hivyo, Jaji Mohammed alisema hajapokea rasmi maombi ya waleta maombi hayo.

Alitaka wadaiwa wengine katika shauri hilo, Mwanasheria Mkuu waSerikali (AG) na TLS waandikiwe mwito wa kuitwa mahakamani.

“Application sijaiona, siwezi kuzungumza chochote, inaonekana TLS wahusika wake wako Dar es Salaam, ni muhimu wakapewa mwito wa kuitwa mahakamani,” alisema Jaji Mohammed na kuongeza kuwa shauri hilo litaendelea kesho na kutaka AG na TLS wawepo mahakamani na maombi ya kutaka kuunganishwa kwenye shauri hilo yatasikilizwa na kutolewa maamuzi.

Akizungumza nje ya mahakama, Lissu alisema wamefanya uamuzi huo kama njia ya kuuongezea nguvu upande wa wadaiwa kutokana na kesi iliyofunguliwa na Wasonga.

Alisema uchaguzi huo umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu na watu wengi huku akibainisha kuwa kuna kile alichokiita njama dhidi ya kuuharibu uchaguzi.

“Baada ya kupata fununu kesi imefunguliwa tukafuta nakala, lakini madai yaliyopo hayana mashiko kwani zaidi ya miaka 65 TLS ipo, lakini jambo la kupinga uchaguzi ndio linajitokeza sasa,” alisema Lissu na kudai `figisu figisu’ za uchaguzi huo ni baada ya kuona wagombea wa safari hii wataleta mabadiliko kutokana na TLS kuwa mfu miaka mingi.

Alisema mambo yenye uhusiano na kikatiba na kisheria yamekuwa yakipita bila TLS kuwa na mchango wowote. Alisema wenye hofu wamejitokeza na kudai wanasiasa wamevamia uchaguzi huo.

“Sheria zilizoanzisha TLS hazina katazo la aina hiyo, sifa kubwa ni wakili anayelipa ada na kupata hati ya kufanya kazi mahakamani,” alidai.

Kwa upande wake, Wakili Wasonga alisema kuna kanuni ambazo zinakinzana na sheria za TLS .

“Baada ya kuzisoma kanuni niliona zinakinzana na sheria za TLS, zimekuwa za kibaguzi hazitoi fursa na nafasi sawa katika kugombea, hazitoi mwanya wa kukata rufaa,” alieleza Wasonga na kubainisha kuwa baada ya Lissu na Masha kupeleka mahakamani maombi ya kuunganishwa kwenye shauri hilo, mahakama itaona wanastahili au la.

No comments:

Post a Comment