KIPAJI ni zawadi kutoka kwa Mungu, lakini inawezekana kuna watu wengi wana vipaji na hawajawahi kuvigundua ni vya kitu gani.
Kitaalamu
inaonyesha hivi, mara nyingi kipaji cha mwanadamu hujulikana kulingana
na anavyopewa nafasi ya wazi kufanya jambo fulani.
Anayefanya
jambo kwa uhuru akiwa na umri mdogo anakuwa na nafasi ya kuonyesha
uwezo wake au kipaji alichonacho na kuanzia hapo, ndipo walio karibu
yake wanakuwa na nafasi ya kukiendeleza.
Asilimia
72 ya wanaofanya vizuri kupitia vipaji walipewa nafasi wakiwa wadogo.
Asilimia 16 tu ndiyo vipaji vyao viligunduliwa na watu wengine kutokana
na umakini wao lakini asilimia 81, wamegunduliwa vipaji vyao wakiwa
wamechelewa kabisa na asilimia 12, walichelewa lakini bado vipaji vyao
vikaweza kutumika.
Inawezekana
kabisa, watoto wengi wa Kitanzania vipaji vyao vimepotea kutokana na
malezi ya aina moja ya Watanzania wengi na wazazi kuendelea kuiga
yaleyale waliyoyaona kwa wazazi wao bila ya kuwa na ubunifu wao binafsi
ili kuboresha maisha kulingana na wakati husika.
Oratilwe Hlongwane ametimiza miaka minne na ushee na sasa yeye ndiye binadamu tajiri zaidi kuliko yeyote katika familia yao.
Anaingiza
mamilioni ya fedha kupitia katika makampuni mbalimbali yakiwemo makubwa
ya utengenezaji wa magari kutokana na ubora wa kazi yake.
Hlongwane
ni mchezesha muziki, maarufu zaidi kama Disco Joker au DJ na
anajulikana dunia nzima sasa kwa jina la utani la DJ Arch Jr.
DJ
Arch Jr aliyeanza kujulikana kwa jina la DJ AJ, ameingia mkataba na
Kampuni ya Kimarekani ya kutengeneza “Headphones” na “Earphones” ya
Beats. Mmiliki wake ni mwanamuziki nguli wa hip hop na milionea, Dr Dre.
Si
kazi rahisi kuingia mkataba na kampuni hiyo lakini hii inatokana na
namna DJ Arch Jr alivyoweza kuonyesha kipaji chake cha kuchezesha
muziki, akianzia kupata umaarufu katika Tamasha la South Africa Got
Talent ambalo aliibuka mshindi akiwa na umri wa miaka mitatu tu na
kubeba kitita cha Rand 500,000 (Sh milioni 87.3).
Pia
DJ Arch Jr ana mkataba na Kampuni ya Djay Software ambayo hutumika
kujifunzia masuala ya Udj. Kampuni nyingine ni Guess Kids pamoja na Mini
Cooper ambao wanatengeneza magari ya aina hiyo.
Hii
inamfanya kuwa mtoto tajiri zaidi nchini Afrika Kusini kwa kuwa kwa
mwaka anaingiza hadi Rand milioni 19 (Sh bilioni 3.3) kupitia mikataba
yake na ana uwezo wa kuingiza hadi Rand milioni 25 (Sh bilioni 4.3) kama
atajumlisha fedha anazolipwa kwenye shoo zake.
DJ
Arch Jr anatokea katika familia ya kawaida kabisa. Baba yake mzazi Glen
Hlongwane ambaye ni mwalimu wa sarakasi aliamua kununua kompyuta
mpakato au ipad kwa ajili ya kukuza uelewa kwa mwanaye mdogo akiwa na
mwaka mmoja tu.
Aliona
kwa kuwa anapenda muziki, basi ni vizuri kuweka ‘application’ ya
kufundisha Udj ya DJ App. Taratibu akawa anaitumia na baadaye akaonekana
kuipenda sana. Mara nyingi alikuwa busy akichezesha kichwa na kumfanya
asiwe na marafiki zaidi ya kuitumia.
Mama
yake mzazi, Refiloe Marumo anasema mwanaye DJ Arch Jr alikuwa
akiwashangaza awali na alikwenda akizidi kujifunza hadi baba yake
alipompa ruhusa kutumia mashine ya Udj aliyokuwa akifanyia mazoezi kama
sehemu ya kujifurahisha.
Baba
yake alinunua mashine hiyo kwa kudunduliza sana fedha zake ili apate
muda wa kuwa nyumbani na familia yake wakati akiichezea.
Alianza
kushangazwa na DJ Arch Jr alipokuwa akifanya vizuri na kutumia muda
mwingi zaidi akiichezea. Ajabu zaidi akawa anajua kuchagua aina ya mpya
za muziki au unaotamba kipindi husika.
Wazazi
wake baadaye walianza kupata lawama kwa majirani na watu wa eneo
walilokuwa wakiishi kwamba wanamfanya mtoto wao kama mtaji.
Wao
walisema hawamlazimishi, akikua ana uwezo wa kuchagua kazi anayotaka,
wataendelea kumpa nafasi ya kufanya anachotaka na kumuunga mkono juu.
Wanadamu hawaishi lawama, kila utakachofanya bila kujali kizuri au kibaya, watalaumu.
Kipaji
cha DJ Arch Jr, sasa kinaiendesha familia yake ambayo imehamia katika
eneo lenye makazi bora jijini Johannesburg ukilinganisha na walivyokuwa
wakiishi awali na hii yote kwa kuwa walitoa nafasi kwa mtoto wao kipaji
chake kuonekana. Kama wewe ni Mzazi Mtanzania, lifikirie hili.
Sasa wasanii wakubwa wa Marekani wenye fedha nyingi, wanatamani kufanya naye kazi katika siku za usoni.
No comments:
Post a Comment