TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI
Chama cha Wananchi CUF kimepokea taarifa ya hatua ya Rais Magufuli
kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kumuondoa Mheshimiwa Nape
Nnauye katika nafasi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
kwa mshtuko na masikitiko makubwa.
Mhe. Nape ameondolewa kwenye Baraza la Mawaziri kibabe na bila aibu
kutokana na kusimamia Haki, Uhuru, Uwajibikaji, Nidhamu na Maadlili ya
uendeshaji wa vyombo vya habari nchini jambo ambalo ni jukumu la msingi
la Wizara yake.
Sote tunatambua kwamba Utenguzi huo unatokana na Mhe. Nape kufuatilia
tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha Clouds Media
Group kinyume na taratibu, maadili na Nidhamu ya utendaji wa majukumu
yake. kitendo hicho pia ni kosa la jinai lisilovumilika.
Kwa niaba ya Chama cha Wananchi CUF, napenda kutumia fursa hii kulaani
mwenendo wa Rais Magufuli wa kuitumia nafasi yake kwa namna inayokosa
BUSARA na HEKIMA ya uongozi kwa TAASISI ya URAIS.
Kitendo cha Rais kumlinda mtuhumiwa ambaye amefanya makosa ya wazi
kabisa kinadhihirisha namna Rais asivyo na utayari wa dhati na uwezo wa
kusimamia nidhamu ya watendaji serikalini.
Huko nyuma na mara kadhaa, Rais Magufuli alichukua hatua za haraka sana
kuwafuta kazi watumishi na watendaji wa serikali waliofanya makosa
madogo mno hata kama ilikuwa ni kimatamshi tu au maamuzi ya bahati
mbaya.
Mifano mizuri ni pamoja na Mhe. Anne Killango (aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga), Dr. Mwele Malecela (aliyekuwa anaongoza taasisi muhimu ya
utafiti wa magonjwa ya binadamu), Wilson Kabwe (Mkurugenzi wa Jiji la
Dar Es Salaam) ambaye alituhumiwa mkutanoni na kufukuzwa hapo hapo bila
kuwepo wala nafasi ya kujitetea.
The Civic United Front (CUF) inashangazwa na maamuzi ya sasa ya Rais
Magufuli ya kumlinda mtuhumiwa wa makosa makubwa na ya wazi kabisa na
kisha kumfukuza kazi Waziri aliyekuwa akitekeleza wajibu wake ili
kulinda heshima ya serikali.
Kwa kitendo hiki cha Rais, CUF inaungana na watanzania wote kuamini kuwa
Rais Magufuli hana nia njema ya kurejesha nidhamu serikalini, na kwamba
yuko tayari kuwalinda vijana wake wachache kuliko kuilinda serikali na
heshima ya nchi na Taasisi ya Urais. Rais anashusha hadhi ya Ikulu na
sasa ikulu imegeuka kuwa mtetezi mkuu wa watumishi waovu wa umma.
CUF itatangaza hatua nzito hapo baadaye, kwa niaba ya chama natumia
fursa hii kumfariji na kumtia nguvu Mhe. Nape kwa ujasiri aliouonyesha
na kusimamia kile ambacho ni haki kwa Taifa, wananchi na sekta ya
habari.
Namuomba asirudi nyuma kutetea haki za watanzania wote na kamwe
asikatishwe tamaa na kitendo hicho kilichokosa utu na heshima, na kujali
mchango mkubwa wa kisiasa ndani ya Chama chake na serikali ya awamu ya
Tano.
CUF inaungana na watanzania wote kulaani kitendo hicho na kwamba
tutakutana pia na vyama washirika katika UKAWA ili kuamua hatua kubwa za
pamoja dhidi ya ukosefu wa haki na Demokrasia nchini na matumizi mabaya
ya mamlaka.
"CUF NI TAASISI IMARA YENYE VIONGOZI MAKINI"
HAKI SAWA KWA WOTE
JULIUS MTATIRO
MWENYEKITI WA KAMATI YA UONGOZI
CUF-TAIFA.
23 Machi, 2017.
No comments:
Post a Comment