Mkurugenzi wa kampuni ya Azimio Housing Estate, Mohamed Ikbal, ambaye
hivi karibuni alimgawia ardhi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda amehojiwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kughushi nyaraka za
Serikali.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro
alithibitisha jana kwamba mfanyabiashara huyo aliitwa kwa ajili ya
mahojiano, lakini aliachiwa kwa dhamana baada ya muda kuonekana
hautoshi.
“Alikuja na wakili wake, lakini ameachiwa kwa dhamana ataripoti siku
nyingine (hakutaja siku),” alisema Sirro. “Anatuhumiwa kughushi nyaraka
za Serikali na sasa upelelezi unaendelea.”
Mfanyabiashara huyo inadaiwa kuwa aliripoti polisi jana saa tano asubuhi na kuhojiwa kabla ya kuachiwa kwa dhamana jioni.
Kuhojiwa kwa Ikbal, ambaye kampuni yake iliwahi kushirikiana na Shirika
la Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika miradi kadhaa tata ya ujenzi, kumekuja
siku chache baada ya kumgawia Makonda eneo la ekari 1500 katika
kitongoji cha Ligato kijiji cha Kisarawe II wilayani Kigamboni kwa ajili
ya viwanda vidogo vidogo.
Siku mbili baadaye, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi aliibuka na kueleza kwamba eneo aliloligawa
mfanyabiashara huyo si lake bali linamilikiwa na serikali na wanakijiji.
“Eneo lile ni la Serikali si la yule mtu aliyejitangaza anampa Makonda
na kwa sababu amemdanganya na mimi ndiye msimamizi wa ardhi, nitamsaidia
Makonda kuchukua hatua ili watu wasijipendekeze kusafisha maovu yao kwa
kutumia migongo ya viongozi,” alisema Lukuvi.
“Hadi siku ile alipokuwa anajipendekeza kwa Makonda, ardhi ile haikuwa
yake, wananchi walishashinda kesi mahakamani kwa sababu hakuwa na
vielelezo. Ukimdanganya Mkuu wa Mkoa umeidanganya Serikali. Makonda
hakuomba ile ardhi ila yeye (Ikbal) ndiye alikwenda kumgawia na
amemgawia akijua kwamba alishashindwa kesi,” alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa hukumu ya kesi hiyo Na 147 ya mwaka 2015 iliyofunguliwa na
Ikbal katika Baraza la Ardhi la Wilaya ya Temeke dhidi ya Baraza la
Ardhi la Kijiji, mfanyabiashara huyo alishindwa.
“Maombi haya yanatupiliwa mbali pamoja na gharama,” ilisema hukumu hiyo ya Januari 13, 2016.
Ijumaa iliyopita mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwakilishi wa Ikbal,
Kamugisha Katabaro aliibuka na kudai Lukuvi amewasikitisha Watanzania na
wataalamu mbalimbali wanaofahamu ukweli wa jambo hilo.
Katabaro alidai Ikbal anamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 3,500 ambayo
aliinunua tangu mwaka 2005 kutoka kwa wananchi wa eneo la Lingato.
“Wananchi waliliuza hilo eneo bila ya kushurutishwa kwa kufuata taratibu
za kisheria na umiliki wa ardhi,” alidai.
Mwananchi lilimfuata siku hiyo, Waziri Lukuvi aweke wazi kuhusu mmiliki
halali wa eneo hilo naye alisema, “Kama mfanyabiashara huyo anaona
ameonewa akate rufaa mahakamani.”
Alisisitiza kuwa eneo hilo ni la serikali na watu waliodhulumiwa
wameanza kuorodhesha majina yao na wataalamu wa ardhi wapo kwenye eneo
hilo wakiendelea na upimaji. “Hiyo ardhi ataipateje wakati mimi ninayo,
na kama ana nyaraka zinaonyesha ameshinda mbona hataki kuonyesha anataka
kuudanganya umma?” alihoji Lukuvi.
Juhudi za kumpata Ikbal hazikuzaa matunda lakini alipoulizwa Katabaro
kuhusu mkurugenzi huyo kuitwa polisi alisema ni kweli alitii wito kama
alivyotakiwa na polisi. Taarifa kwamba alikamatwa siyo za kweli kwani
alihojiwa na kutoka jana jioni baada ya kuwasili kituoni hapo saa tano
asubuhi jana,” alieleza.
Eneo jingine ambalo Azimio ilizua utata ni umiliki wa ardhi na
uthaminishaji wake kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa uitwao
Dege Eco Village, Kigamboni. Ulisimama Februari mwaka jana kutokana na
utata wa ubia.
No comments:
Post a Comment