DAR ES SALAAM: Mtindo wa maisha ya kisasa kwa wasichana Bongo, yamedaiwa
kuwa yatasababisha upofu kwa akina dada kadhaa, wakiwemo Wema Sepetu,
Jacqueline Walper Masawe ‘Wolper’, Aunt Ezekiel na wenzao kwa sababu ya
kuvaa macho bandia pasipo ushauri wa daktari.
Katika siku za hivi karibuni, umezuka mtindo wa wasichana wa kisasa
kujipamba kwa urembo wa aina mbalimbali, lakini sasa, wameanza kuvaa
macho bandia machoni mwao na hivyo kuyafanya kuonekana kama ni ya
kizungu.
Risasi Mchanganyiko lilifanya jitihada za kuwatafuta wataalamu wa afya,
hususan macho na kufanikiwa kukutana na daktari Godfrey Chale, ambaye
baada ya kuelezwa suala hilo, alitoa ufafanuzi kuhusu kitu kinachoweza
kuwakuta watu wote wanaopenda kuvaa macho hayo ya bandia.
“Kuna kitu kinaitwa Conduct Lance, hizi zinatolewa hospitali kwa watu
wenye uhitaji nazo. Huwekwa na madaktari kwa namna ambayo inamfanya
mvaaji awe comfortable (ajisikie vizuri), kama hawa watakuwa wanapatiwa
huduma hiyo hospitalini haina tatizo, lakini kama wanavaa kienyeji, iwe
saluni au nyumbani, ni hatari kubwa kwao.
“Macho ya kila mmoja yana namba na nguvu tofauti ndiyo maana hata
wanaovaa miwani wanapaswa kupimwa ili kujua watapewa miwani namba ngapi.
“Kila mtu macho yake yana nguvu tofauti, kwa hiyo unapopimwa, wanajua
upewe miwani ipi, sasa ile wanayovaa wao haina tofauti na miwani, kwa
hiyo wanapaswa kupimwa ili ziwe sawa na nguvu za macho yao.
“Ukivaa miwani bila kujua nguvu za macho yako ni hatari kwa sababu kama
lensi zina nguvu, zinaua macho yako. Unajua kadiri mtu anavyokua, ndivyo
nguvu ya viungo mbalimbali mwilini vinavyopungua nguvu zake. Sasa kama
nguvu ya macho yako ni ndogo au kubwa na unavaa miwani yenye nguvu kubwa
au ndogo, inaua macho yako.
“Kwa hiyo uwezekano mkubwa wa macho hayo kwisha nguvu ndani ya muda
mfupi. Mbaya zaidi kama macho hayo wanajiwekea wenyewe bila utaalamu,
wanahatarisha afya ya macho yao,” alisema daktari huyo.
Mtaalam huyo alisema hata miwani za jua zinazovaliwa, wahitaji
wanashauriwa kwenda kununua katika maduka yenye wataalam badala ya
kununua barabarani. Alisema katika maduka hayo, zipo ambazo ni salama
kutokana na vipimo.
“Maana pia kuna miwani zingine zipo ambazo zinabadilika kulingana na
hali. Wakati wa jua zinageuka kuwa nyeusi kama ya jua na usiku zinakuwa
za kawaida, ndiyo maana unaona kuna watu wanavaa miwani hadi usiku, ni
hizi za namna hii,” alisema Dk Chale.
Wakizungumzia kuhusu madhara ya uvaaji wa macho hayo bandia, baadhi ya
mastaa walieleza kushtushwa kwao na athari hizo, huku wengine wakisema
siyo rahisi wao kudhurika, kwa vile wanatumia za bei mbaya.
Muigizaji wa filamu ambaye pia ni video queen, anayejulikana kama Lulu
Mdogo, alisema mara chache huvaa macho hayo katika ishu maalum, ingawa
anajua kuwa yana madhara.
Kwa upande wake, Lulu Diva alikiri kuwa mpenzi wa kuvaa macho hayo na
kuweka wazi kuwa yamekuwa yakimpa taabu kwani macho yake huuma mara kwa
mara. Shoga wa zamani wa Wema Sepetu, Muna ambaye pia huvaa macho hayo,
alisema amefanya hivyo mara nyingi na hajawahi kuona jambo lolote baya
juu ya macho hayo.
“Macho ninayovaa mimi ni ya kiwango cha juu, hayana madhara kabisa, yapo poa tu,” alisema.
Aunt Ezekiel naye pia alisema ni miongoni mwa wavaaji wakubwa wa macho
hayo na kwa muda wote hajawahi kupata madhara ya aina yoyote huku Wolper
akisema ameanza muda mrefu kuyavaa hajaona madhara kwa kile alichodai
ni kwa vile yake huwa ni ya kiwango cha juu kuliko wengine.
No comments:
Post a Comment