Thursday, February 16, 2017

TIGO MATATANI KUHUSU HISA

Mawakili wa wajibu maombi katika kesi ya utata wa hisa za Tigo wamedai kuna tuhuma dhidi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Pamela Mazengo, Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA) na mfanyabishara maarufu wa Dar es Salaam ya kula njama ya kughushi na rushwa.

Mawakili hao wanaiomba mahakama hiyo kuwaita  watuhumiwa kwa ajili ya kujieleza kuhusiana na tuhuma hizo ili mahakama ijiridhishe.

Hoja hizo ziliwasilishwa mahakamani jana mbele ya jopo la majaji watatu, Jaji Mbarouk Mbarouk, Augustine Mwarija na Jaji Shaaban Lila.

Jopo hilo lilitakiwa kupitia mwenendo wa Mahakama Kuu kuhusu shauri hilo, lakini lilikwama kufanya hivyo kwa sababu mawakili wa wajibu maombi, Golden Globe na Quality Group waliwasilisha pingamizi la awali.

Waombaji katika shauri hilo ni Millicom (Tanzania) NV ambao wanawakilishwa na Wakili Erick Ng’amaryo, Fayaz Bojan, Gaudiosus Ishengoma na Audax Kahendaguza.

Wajibu maombi ni James Bell, Golden Globe na Quality Group wanaowakilishwa na Wakili Kamala Mpaya, Joseph Ndazi, Daniel Welwel, Nduruma Majembe na Hurbert Nyange.

Akiwasilisha pingamizi hilo, Wakili Majembe alidai kuna hukumu mbili hazipo katika jalada la shauri hilo, kuna tuhuma za kughushi kinyume cha taratibu na sheria.

Alidai awali mwombaji alisomeka Millicom International lakini sasa inasomeka Millicom Tanzania NV na kuna kumbukumbu ambazo hazipo.

Alidai Pamela Mazengo, mfanyabiashara wa Dar es Salaam na Brela hawapo mahakamani kujibu tuhuma za kula njama, kughushi na rushwa hivyo wanatakiwa kuitwa.

Brela inatuhumiwa kinyume cha sheria kubadili usajili wa Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo huku mfanyabiashara huyo akituhumiwa kuisababishia hasara kampuni hiyo, hivyo wanatakiwa kupewa nafasi ya kujibu tuhuma dhidi yao.

“Ni ombi langu mahakama iwaunganishe katika shauri, Brela, mfanyabiashara, Mazengo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,”alidai.

Wakili Nyange akiwasilisha pingamizi alidai mahakama haina kizuizi chochote cha kuwaunganisha wanaotumiwa  na kwamba mahakama hiyo ya juu inapitia mwenendo halisi wa shauri.

Mawakili wengine Joseph Ndaza, Kapaya walishauri jopo hilo kuwaita watuhumiwa kwa sababu tuhuma nzito na misingi inaeleza wazi kwamba anayetuhumiwa anatakiwa kuitwa kujieleza ili mahakama ijiridhishe.

Akijibu hoja hizo, wakili wa mwombaji, Ng’maryo alidai walichowasilisha wajibu maombi si pingamizi na kwamba pingamizi linatakiwa kuwa katika misingi ya kisheria.

Alidai mahakama hiyo ya juu ilijielekeza kuitisha jalada la shauri hilo kwa ajili ya kulipitia kuona Mahakama Kuu ilifanya nini na wala si kuangalia wahusika katika shauri.

Wakili huyo alisema kitendo hicho kinachotakiwa kufanywa na mahakama kinaitwa Self Movement of the Court (SUO MOTTU) na inapoamua kufanya hivyo haina sababu hata ya kuwaita waombaji wala wajibu maombi.

“Mahakama inaweza kuendelea kupitia yenyewe hata bila wahusika kuwepo, pingamizi haliwezi kuwasilishwa katika hatua hiyo na kwamba wahusika kuanza kuzuia Mahakama ya Rufaa kufanya SUO MOTTU ni kujichanganya,” alidai na kuongeza kwamba hatua hiyo haiwezi kuzuiwa na upande wowote.

Awali kabla ya kuwasilishwa kwa pingamizi mawakili wa wajibu maombi walitaka shauri lisisikilizwe kwa sababu mjibu maombi wa kwanza, James Bell hakuwepo mahakamani wala mwakilishi wake.

Kapaya alidai taarifa ya kumwita mahakamani ni tofauti na kilichopo mahakamani kwani kilichokuwepo mahakamani ni kupitia mwenendo wa shauri wa Mahakama Kuu lakini hati ya kumwita inaeleza hukumu na kikaza hukumu.

Pia alihoji mfumo uliotumika kuwasilisha hati hiyo ya wito kwamba haukuwa sahihi kwani walitumia magazeti hivyo waliomba utumike utaratibu sahihi ili aweze kuhudhuria katika shauri hilo kwani ni mtu muhimu.

Wakili  Faya akijibu alidai kinachofanywa na mawakili wa wajibu maombi wa pili na watatu ni mbinu za kuchelewesha kesi kwa sababu waliamua kufanya hivyo kutokana na historia ya Bell.

Alidai walitangaza katika magazeti mbalimbali likiwamo Dailynews na Gurdian la Uingereza.

Baada ya kusikiliza hoja hizo jopo liliamua kuendelea kusikiliza pingamizi la awali lilowasilishwa na wajibu maombi bila mwombaji wa kwanza bell kuwepo.

Msingi wa shauri hilo ni kwamba Bell aliwahi kufungua kesi dhidi ya Tigo, Millicom International, Kampuni ya UFA Ltd na MIC Tanzania Limited na katika usikilizaji mahakama ilitoa uamuzi wa upande mmoja kwa sababu upande wa utetezi walishindwa kuwasilisha utetezi dhidi UFA na Millicon.

Bell alianza mchakato wa kukazia hukumu , mwaka 2009 maombi yake yalikataliwa na Jaji Kalegea kwa sababu hisa hizo si za Millicom na UFA.

Mwaka 2014 Bell aliomba kukazia hukumu ambapo Novemba mwaka huo Mazengo akateua kampuni ya udalali kwa ajili ya kuuza hisa  na hisa zikauzwa.

Baada ya kuuzwa kwa hisa hizo ndipo alipojitokeza Millicom Tanzania NV akadai yeye ndiye mwenye hisa hizo hivyo Mazengo alitoa hati nyingine ya kuuza hisa, uhamishaji wa hisa ukafanyika.

Millicom NV aliwasilisha malalamiko akidai kwamba hakuhusishwa tangu mwanzo wa shauri hilo badala yake anaingizwa katika hatua za mwisho.

Malalamiko hayo yakaifanya Mahakama ya Rufaa kujielekeza kuitisha jalada la shauri hilo kwa ajili ya kulifanyia mapitio kuona Mahakama Kuu ilifanya nini.

No comments:

Post a Comment