Friday, February 10, 2017
MZEE WA UPAKO AFUNGUKA ASKOFU GWAJIMA KUTAJWA
Dar es Salaam. Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ ameshauri kuwapo kwa utaratibu maalumu wakati wa kuwaita kwa mahojiano watu wanaoitwa kwa mahojiano kuhusu dawa za kulevya.
Mzee wa Upako alisema hakukuwa na umuhimu wa vyombo vya habari kuhusika katika kuwataja watu hao hasa viongozi wa dini, bali wangeitwa kwa barua maalumu. Alisema inapotokea wachungaji wakahusishwa na dawa za kulevya ni muhimu kuwapo na ushahidi wa kutosha kinyume na hapo, itawavunjia heshima yao.
Mzee wa Upako alisema anaunga mkono kwa asilimia zote vita dhidi ya dawa za kulevya ila hajafurahishwa na namna suala hilo linavyofanyiwa kazi hali inayoweza kuwaharibia watu heshima.
“Kujenga heshima ni kazi kubwa sana inaweza kuchukua muda mrefu kuirudisha kama ilivyokuwa. Utakuta mtu ametumia muda mrefu kujenga jina lake halafu unakuja kumharibia, maisha ya mtu ni heshima yake, itamvuruga kwa muda na kumuachia kidonda kikubwa kujenga upya heshima yake.
“Binafsi sioni sababu ya vyombo vya habari kuhusika katika suala hili, ndiyo maana nasisitiza ni muhimu kuwa na ushahidi siyo kumtuhumu bila uthibitisho.”
Alisema ni vyema taratibu za kisheria zikafuatwa na ngazi husika zikachukua jukumu hilo bila kuingiliwa.
“Usalama wa nchi una intelejensia zake, naamini watu wa usalama wangeshughulikia suala hili kupitia Kamanda Siro au Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya wao wanajua wanafanya vipi kazi yao, huwezi kwenda kwenye vyombo vya habari kumuita unayemshuku,” alisema. Akizungumzia sakata la Josephat Gwajima kutajwa kwenye orodha hiyo, Mzee wa Upako alisema hayo yaliwahi kumkuta yeye mwaka 1997.
“Niliwahi kutajwa nauza dawa za kulevya mwaka 1997. Askari walitumia busara nikaitwa makao makuu ya Polisi wakaniambia natuhumiwa, nikawaambia fanyeni uchunguzi. Walipogundua kuwa sina makosa wakaamua waniache. “Niliishi miaka saba wachungaji wenzangu wakininyanyapaa kila nilichofanya ilionekana ni dawa za kulevya. Ilitumia muda mrefu kusafisha jina langu,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment