Akizungumza jana baada ya mazoezi ya yaliyofanyika kwenye Uwanja wa
shule ya Sekondari Igawilo, nje kidogo ya jiji la Mbeya, Ngassa alisema
kwamba hajakatishwa tamaa na matokeo ya mchezo uliopita dhidi ya Prisons
kwa sababu yalitokea kwenye hali ya mchezo na ni jukumu la benchi la
ufundi kurekebisha makosa yote kabla ya kusaka pointi tatu kwenye mchezo
dhidi ya JKT Ruvu.
“Huwezi kukata tamaa kwa matokeo ya mechi moja, jambo zuri ni kujipanga
upya ili tuwe tayari kwa mchezo unaofuata, binafsi bado nina imani kubwa
na timu yetu, tutafanya vizuri kwenye michezo yote iliyosalia na
kumaliza ligi tukiwa kwenye nafasi za juu, tuna kikosi kizuri na kila
mchezaji ana kiu ya kufanya vyema ili kuisaidia timu," alisema Ngasa.
Aidha, akizungumzia juu ya mchezo wa kesho dhidi ya JKT Ruvu, Ngassa
alisema hafahamu vizuri uwezo wa timu hiyo kwa sasa na ni ngumu kwake
kubashiri matokeo.
“Siifahamu vizuri kwa sasa JKT Ruvu, ila naamini itakuwa bado ni timu ya
ushindani kwa sababu iko kwenye ligi, jambo muhimu kwetu ni kujiandaa
vizuri na tumefanya hivyo," aliongezea kusema Ngasa.
Katika hatua nyingine, Ngassa ametoa pongezi kwa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) kwa kujitahidi kupiga hatua katika soka la vijana, licha
ya changamoto kubwa zinazolikumba Shirikisho hilo hasa kwenye upangaji
wa ratiba ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza.
“Nadhani TFF wanafanya vyema, nchi nyingi duniani zimeendelea kisoka kwa
kuwekeza kwenye soka la vijana, changamoto ziko nyingi lakini ni vyema
waendelee kufanya kile wanachokifanya sasa kwa sababu muda si mrefu
Watanzania wataona matunda yake,”alisema Ngasa.
No comments:
Post a Comment