Uamuzi
uliofanywa wiki iliyopita na Waziri wa Maliasili na Utalii, Professa
Jumanne Maghembe wa kuagiza kuendelea mchakato wa kulitenga eneo la pori
tengefu la Loliondo umepingwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Badala
yake, RC Gambo ameagiza Kamati ya wataalamu iliyoundwa kwa maelekezo ya
Waziri Mkuu, Khasimu Majaliwa inayochunguza chanzo cha mgogoro wa
Loliondo iendelee na kazi iliyopewa na hatimaye itoe mapendekezo yake ya
namna ya kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa miongo miwili.
Gumbo
alikuwa akizungumza jana katika mkutano wa wadau wa vyombo vya habari
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Alisema
hakuna kiongozi yeyote mwenye mamlaka ya kukosoa au kusimamisha maagizo
ya Waziri Mkuu isipokuwa Makamu wa Rais na Rais.
RC
Gumbo alionekana dhahiri kuwa amekerwa na kukasirishwa na uamuzi wa
Waziri Maghembe wa kufanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Loliondo
na kutoa maagizo ya kugawa eneo la kilometa za mraba 1500 kuokoa
Hifadhi ya Serengeti.
Alisema
uamuzi uliotolewa na waziri huyo ni ushauri kwa kamati yake na jambo
linalozusha sintofahamu juu ya mwenye mamlaka zaidi kati ya Waziri na
Mkuu wa Mkoa .
“Hakuna kiongozi mwingine yeyote mwenye kukosoa maagizo au maelekezo ya Waziri Mkuu isipokuwa Makamu wa Rais na Rais.
“Sisi kauli ya waziri tunaichukulia kama ushauri ambao unaweza kutolewa na mwananchi yeyote, ” alisema.
Alisema
ni lazima kamati ya wataalamu aliyoundwa ikamilishe kazi yake ikiwa ni
pamoja na kujiridhisha kuhusu mipaka, vyanzo vya maji, maeneo ya
ufugaji, uhifadhi, mipaka ya vijiji na hatimaye kuwasilisha mapendekezo
yake serikalini yafanyiwe kazi na si vinginevyo.
Mkuu
huyo wa Mkoa alishangazwa na uelewa na umakini wa Wizara ya Maliasili
na Utalii katika kulitambua na kufuatilia eneo la pori tengefu.
RC Gumbo alisema inaelekea wataalamu wa wizara hawana uelewa wowote kuhusu kinachoendelea Loliondo.
“Wizara
inazungumzia pori tengefu lakini tayari kuna mji pale, hata eneo la
kilometa za mraba 1500 wanazosema tumewauliza inaanzia wapi na kuishia
wapi hawajui.
"Hata aliyechora ramani naye hajui mipaka ndiyo maana nasema tuache kamati imalize kazi yake," alisema.
No comments:
Post a Comment