Mbunge
wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), amesema kitendo cha makatibu wakuu,
wakuu wa mikoa na wilaya kuvaa sare za Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, ni kinyume na Katiba ya
nchi na kwamba ni dalili ya nchi kuendeshwa kijeshi.
Tangu
alipoapishwa Novemba 5 mwaka juzi, Rais John Magufuli amekuwa na
utaratibu wa kuteua maofisa JWTZ katika nyadhifa mbalimbali jambo ambalo
wabunge wa Upinzani wamekuwa wakilipinga mara kwa mara.
Waitara
alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akiomba Mwongozo, baada ya
kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, akisisitiza kuwa wanajeshi
hao kufanya shughuli za kisiasa si sawa.
Huku
akitumia kanuni ya Bunge ya 68 (7) na kurejea taarifa ya habari ya
Shirika la Utangazaji (TBC) alisema: “Wakati naangalia taarifa ya habari
nikamwona Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Milanzi
(Meja Jenerali, Gaudence) akifanya shughuli zake huku amevaa kijeshi
kinyume cha Ibara ya 147 ya Katiba yetu.”
Baada
ya kikao cha Bunge kuahirishwa saa 7 mchana, Waitara alisema kuwa ni
kawaida kwa wateule wa Rais kuvaa sare hizo na kusisitiza: “Wakuu wa
mikoa ni wanasiasa na ndani ya CCM ni wajumbe wa kamati za siasa za
mikoa. Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya, sasa
wanaanzaje kuvaa au kujihusisha na mavazi ya kijeshi?”
Akiwa
bungeni, Waitara alisisitiza kuwa siku za karibuni Mkuu wa Wilaya ya
Kakonko, Kanali Hosea Ndaga naye alionekana akifanya shughuli zake huku
amevaa sare hizo.
“Ukisoma
Katiba pamoja na mambo mengine, inapiga marufuku wanajeshi kujihusisha
na siasa. Hawa viongozi wanaovaa nguo za kijeshi wanawatisha wananchi
wanapokwenda kusikiliza matatizo,” alisema.
Ibara
ya 147 (3) inasema: “Itakuwa marufuku kwa mwanajeshi kujiunga na chama
chochote cha siasa, isipokuwa tu kama atakuwa na haki ya kupiga kura
iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba hii”.
Mbunge huyo alihoji: “Inakuwaje wengine wanavaa sare za Jeshi na vyeo juu wakati wamestaafu?”
Akijibu
Mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga alisema kwa mujibu wa
kanuni ambayo Mbunge huyo aliombea Mwongozo, hoja aliyotoa ni suala
ambalo halijatokea ndani ya Bunge wakati likiendelea na shughuli zake,
hivyo asingeweza kutoa majibu yoyote.
No comments:
Post a Comment