Monday, February 27, 2017

MBUNGE AWAOMBA WANANCHI WAMPIGE MAWE

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani maarufu Profesa Majimarefu, ametoa ruhusa kwa wakazi wa jimbo lake kumwadhibu kwa kumpiga mawe iwapo atashindwa kutekeleza ahadi alizoahidi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Majimarefu aliyasema hayo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara na wananchi wa Vijiji vya Kwemshai, Ngulu na Mlungui, katika ziara yake jimboni mwake.

Alisema licha ya kuwa nje ya nchi kwa matibabu, lakini baada ya afya yake kuimarika amerejea nchini akiwa tayari kutatua kero za umma.

Aidha, amewaomba wapigakura wake kuendelea kushirikiana naye huku wakimpatia muda kumwezesha kuwatatulia kero hizo.
 
“Nawashukuru kwa kuniombea pale nilipokuwa nikiugua, nilikuwa nje ya nchi kwa matibabu sala zenu zimeniwezesha kuungana nanyi leo," alisema.

Aliwaeleza wananchi wa Kijiji cha Mlungi kuwa tatizo la maji na umeme viko mbioni kutatuliwa ndani ya mwaka huu na kwamba wale wanaoeneza maneno kuwa hakutafanyika kitu wanajidanganya kwa vile mambo yanakwenda sawa.

Majimarefu alisema katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, ameamua kumkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhandisi Robert Gabriel kusimamia Mfuko wa Jimbo kusaidia miradi.

Katika hatua nyingine, Majimarefu aliwashukia mahasimu wake wa kisiasa aliodai wanatumia mbinu chafu kumchafua kuhusu afya yake tangu alipougua na kwenda kutibiwa nje.

“Kuna mahasimu wangu wa kisiasa wanapita kila kijiji kuzungumzia afya yangu kwamba nimepoteza fahamu na kukatwa mguu, siyo kweli myapuuze,”alisema.

Majimarefu alisema wananchi wapuuze uzushi huo usiokuwa na msingi kwani una lengo la kuwavunja moyo kwa manufaa yao ya kisiasa.

Hata hivyo, alisema kuwa hatavunjika moyo kwa maneno hayo na badala yake yamekuwa changamoto kwake kutekeleza ahadi zake na hafanyi hayo kwa lengo la kujipatia umaarufu kama inavyodaiwa na baadhi ya watu ila ni moja ya utekelezaji wajibu wake kwa wananchi waliomchagua.

Majimarefu aliwaeleza wananchi hao kuwa wakati wa watu kufanya fitna umekwisha na uliobaki ni ule wa kusema ukweli akiwahimiza kufanya kazi sambamba na kulinda rasilimali misitu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Gabriel, alisema kwamba kazi yake ni kusimamia rasilimali za umma, hivyo atahakikisha kwamba yale yote yanayoanzishwa na mbunge huyo anayalinda.

No comments:

Post a Comment