Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema itamchukulia hatua
muwekezaji aliyetoa ardhi kwa serikali ya mkoa wa dar es Salaam kwa
ajili ya ujenzi wa viwanda, kwa madai kuwa ardhi aliyoitoa siyo yake.
Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi, alitoa kauli hiyo jana
jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa muwekezaji huyo aliidanganya
serikali pamoja na kumdanganya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul
Makonda, ambaye ndiye aliyekabidhiwa eneo hilo kwa niaba ya serikali.
Mbali na kosa la kuidanganya serikali, Lukuvi pia alisema atamchukulia hatua mfanyabiashara huyo kwa kumiliki ardhi kinyume cha sheria.
Kuhusu Mkuu wa Mkoa , Paul Makonda, Lukuvi alisema
tayari amekwishafanya naye mawasiliano na kumuelewesha kuwa
alidanganywa kwa kuambiwa kuwa anapewa eneo kwa ajili ya viwanda, huku
eneo lenyewe likiwa ni mali ya serikali.
Siku
ya Jumanne wiki iliyopita Makonda alikabidhiwa ekari 1500 za ardhi na
Mkurugenzi wa Azimio Housing Estate Mohamed Iqbal kwa ajili ya ujenzi wa
viwanda vidogo vigogo nchini, katika eneo la Kigamboni Dar es Salaam.
Akizungumza
mara baada ya makabidhiano hayo eneo la Kisarawe II wilaya ya Kigamboni
Mkurugenzi huyo alisema wameamua kumkabidhi eneo hilo ili kuunga mkono
jitihada za Rais Magufuli za kuijenga Tanzania ya viwanda na kuwakomboa
wananchi wenye uchumi wa kati.
Kwa
upande wake Makonda alieleza kuwa dhamira ya viwanda ya Rais Magufuli
inabidi itafsiriwe kwa vitendo, hivyo eneo hilo litatumika kwa ajili ya
ufugaji, kilimo, usindikaji, utengenezaji wa sabuni na eneo hilo
litatumika na wilaya zote.
No comments:
Post a Comment