Tuesday, February 21, 2017

KOCHA WA TIMU YA TAIFA YA UBELGIJI ASEMA SAMMATTA ANAUWEZO WA KUCHEZA LIGI KUU UINGIREZA


Kocha wa timu ya taifa ya Ubelgiji Roberto Martinez amekiri kuwa, mshambuliaji na nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta ana-ubora wa kucheza ligi kuu ya  England maarufu kama EPL.

Shaffihdauda ilifanya juhudi za kumtafuta kocha huyo ambaye amewahi kufundisha soka England katika vilabu vya Wigan kabla haijashuka daraja pamoja na Everton kabla ya kupewa majukumu ya kuifundisha timu ya taifa ya Ubelgiji.

Juhudi zilifanywa na Mbwana Samatta kuiunganisha shaffihdauda.co.tz na Martinez, hatimaye kocha huyo akatoa ushirikiano. Martinez amesema, Samatta ni mshambuliaji mwenye kiwango kikubwa na uwezo wa kucheza soka kwenye ligi yoyote ikiwemo EPL, pia amesema ameongea na kushauriana vitu vingi na Samagoal.

Shaffihdauda.co.tz: Umeshawahi kumshuhudia Samatta akiwa uwanjani akiitumikia klabu yake ya Genk?

Martinez: Mimi ni kocha wa timu ya taifa ya Ubelgiji kwa hiyo nafatilia kwa karibu sana ligi za hapa kwa hiyo nimeshamuona mara kadhaa akiwa uwanjani.

Shaffihdauda.co.tz: Unaonaje uwezo wake, anaweza kucheza kwenye ligi kubwa zaidi ya Ubelgiji au timu kubwa zaidi ya Genk?

Martinez: Samatta ni mchezaji mzuri mwenye ubora wa kucheza EPL na anaweza kukupa vitu tofautitofauti kwa ubora wa hali ya juu. Lakini anatakiwa achague baadhi ya vitu ambavyo anaweza kuvifanya kwa ubora wa juu zaidi.

Shaffihdauda.co.tz: Kwa jicho lako la kiufundi, unadhi Samatta anatakiwa afanye nini ili kuongeza ubora wake ambao utafanya atoke hapo alipo na kusonga mbele zaidi?

Martinez: Ili kuwa bora sio lazima utumie kila kitu ulichonacho au unachoweza kufanya, kuna wakati inabidi uamue kipi ukipe kipaumbele halafu kingine kifate nyuma.

Shaffihdauda.co.tz: Ni kitu gani kimekuvutia kwake ambacho kama ungekuwa kocha wa klabu kingekufanya umsajili kwenye timu yako?

Martinez: Anajua namna ya uwakimbia mabeki, anatakiwa kufanya zaidi mazoezi ya spidi na akiwa uwanjani anatakiwa kufanya hivyo.

Shaffihdauda.co.tz: Kama Samatta akikuomba ushauri, utamshauri afanye nini ili kuongeza uwezo wake na kumfanya awe bora zaidi ya alivyo sasa kitu kitakachomfanya aonekane na vilabu vikubwa

Martinez: Anaweza kucheza kama target man kwa sababu anaweza ku-drible na kupangua mabeki lakini anatakiwa kuwa na nguvu kwa hiyo anatakiwa kufanyia kazi jambo hilo, pia inabidi achezee sana mpira mazoezini ili kuimarisha uwezo wake wa kumiliki mpira.

Kwa upande wake Mbwana Samatta amesema, amefurahi kukutana na Martinez moja ya makocha wenye mafanikio makubwa kwenye soka. Amepewa ushauri baada ya kuzungumza na kocha huyo na atafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa. Kikubwa zaidi ni kocha huyo kuonekana kuvutiwa na uwezo wa Samatta ikiwa ni pamoja na kukiri anaubora wa kucheza EPL ambayo haswa ndio ndoto ya Samatta.

“Kwangu ni bahati kubwa sana kukutana na kocha mkubwa kama Martinez ambaye amewahi kuwa kocha wa Wigan na Everton zote amezifundisha zikiwa EPL na sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Ubelgiji akiwaongoza wachezaji wenye majina na mafanikio makubwa kwenye soka duniani. Hata ukiangalia kwenye viwango vya FIFA utaona Ubelgiji ni taifa lenye mafanikio kwa sababu lipo kwenye nafasi nzuri.”

“Niliongea nae mambo kadhaa akanishauri vitu vingi vya kuvifanyia kazi mazoezini na kwenye mechi, kwakweli nimefurahi kwa sababu ni mara chache unaweza kupata fusra kama hii ya kukutana na makocha wenye mafanikio kwenye soka duniani halafu wakakubali kukupa ushauri ufanye nini ili ufanikiwe zaidi.”

No comments:

Post a Comment