MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara imeiamuru Kampuni ya Kufua Umeme IPTL
kuilipa Benki ya Standard Chartered Hong Kong na Benki ya Standard
Chartered Malaysia Dola za Marekani 168,800,063.87.
Uamuzi huo ulitolewa na mahakama hiyo baada ya kukubali kuisajili
hukumu iliyotolewa Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara Uingereza ikiitaka
kampuni hiyo kulipa fedha hizo.
Jaji Baker Sehel alitoa uamuzi huo baada ya kuisajili hukumu hiyo hivi karibuni na kuamuru IPTL kulipa fedha hizo.
Alisema walalamikiwa wanaweza kuwasilisha maombi ndani ya siku 21 ya
kutaka usajili huo uwekwe pambeni na taarifa ya kusajili hukumu
iwasilishwe kwa walamikiwa ikionyesha haitatekelezwa mpaka zipite siku
21.
Novemba 16 mwaka jana, Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara Uingereza
ilisikiliza kesi hiyo baada ya walalamikiwa kushindwa kuwasilisha
utetezi wao.
Walalamikaji katika kesi hiyo walikuwa Standard Chartered Bank Hong Kong
Limited na Standard Chartered Bank Malaysia wakati walalamikiwa ni
IPTL, VIP Engeneering and Marketing Limited na Pan Africa Power Limited.
Katika shauri hilo walalamikiwa walishindwa kuwasilisha utetezi kwa
madai kwamba mtambo wa IPTL na yote yanayohusu kampuni hiyo yako
Tanzania na kwamba kabla ya kesi hiyo kuna kesi nyingine mbili nchini.
Inadaiwa msingi wa kesi hizo ni kuhusu uhalali wa Standard Chartered Bank kuwa mdai halalali wa IPTL.
Katika kesi moja, IPTL na PAP wanaidai Standard Chartered Bank Sh
trilioni sita na ya pili, VIP wanaidai benki hiyo Sh trilioni moja.
Pamoja na kuwasilisha pingamizi, mahakama ilitupilia mbali na kusikiliza kesi hiyo upande mmoja.
No comments:
Post a Comment