ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye aliisaidia
Polisi kwa siku tatu kuhusu biashara ya dawa za kulevya, ametishia
kuamuru mapepo anayotoa kanisani yaingie kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda.
Makonda ndiye aliyetangaza kumtaka Gwajima pamoja na jumla ya wanasiasa
na wafanyabiashara 64 kufika Kituo Kikuu cha Kati cha Kanda Maalum ya
Dar es Salaam Ijumaa kwa ajili ya mahojiano kuhusu biashara ya madawa ya
kulevya.
Askofu Gwajima alisema licha ya jina lake kutajwa katika tuhuma hizo
nzito, hana mpango wa kumshtaki Makonda kwa kuwa atakuwa anaishtaki
serikali.
Alisema Makonda ni mteule wa Rais John Magufuli, hivyo kumshtaki Mkuu
huyo wa Mkoa ni sawa na kumshtaki aliyemteua pia na hayuko tayari
kufanya hivyo kwa kuwa anavutiwa na Rais na utendaji kazi wa serikali
yake.
“Mimi najua cha kufanya," alisema Gwajima wakati akizungumzia kanisani
kwake jana, hatua ambazo atachukua nje ya kumshtaki Makonda mahakamani.
"Yesu alipopita mahali, akakuta kuna mtu ana mapepo 2,000, alivyoanza
kuyatoa yakamwambia turuhusu twende kwa wale nguruwe," alisema.
"Sasa sisi mapepo yatakapouliza tutayaambia nguruwe ni nyama yasiende huko, tutayaambia pa kwenda."
Aidha, Gwajima jana aliwaeleza waumini wake yaliyomkuta huku akiwaonyesha nyaraka za ukaguzi baina yake na Jeshi la Polisi.
Alhamisi, Askofu Gwajima alifika kwenye Kituo Kikuu cha Polisi jijini
Dar es Salaam baada ya jina lake kuwa miongoni mwa majina 65
yaliyokuwamo katika orodha ya pili ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam huyo
ya watuhumiwa wa dawa za kulevya aliowataka waripoti polisi Ijumaa.
Lakini Akofu huyo aliamua kuripoti siku moja kabla na kushikiliwa na jeshi hilo hadi juzi.
Askofu Gwajima alifika kanisani hapo majira ya 5:18 asubuhi na kulifanya
kanisa kuzizima kwa shangwe kwa takribani dakika 10 wakati anaingia
huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa kanisani hapo na walinzi wa kanisa
hilo waliokuwa kwenye sare ya suti nyeusi na tai nyekundu na miwani ya
rangi nyeusi.
Nipashe ilishuhudia kanisa hilo likiwa limefurika maelfu ya waumini huku
wengine wakionekana kukosa mahali pa kuketi na kulazimika kusimama na
wengine kuketi kwenye viunga vya nje ya kanisa hilo.
Baada ya Askofu Gwajima kuingia kanisani na kuketi, wasaidizi wake
walitangaza kuwa baada ya kutoa sadaka, Askofu huyo atazungumza nao,
tangazo ambalo 'lililipua' zaidi kanisa hilo kwa shangwe huku baadhi ya
waumini wakishangilia kwa kunyanyua viti.
Utoaji sadaka ulipomalizika, Askofu Gwajima huyo alisimama na kueleza
kuwa kabla ya kuhubiri neno la Mungu, aeleze kwanza kuhusu kilichompata
polisi.
Alisema taarifa za kutakiwa kuripoti polisi alizipata Jumatano wakati
akiwa kwenye chopa lake wakiwa safarini na wenzake kuelekea Dodoma kutoa
huduma ya kiroho.
Askofu Gwajima alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, alimtaka
rubani wake ageuze chopa kurejea jijini Dar es Salaam ili siku
iliyofuata (yaani Alhamisi) aripoti alikotakiwa.
"Nisingeweza kuendelea na safari ya kwenda kutoa huduma kwa sababu
nilikuwa tayari nimeshatajwa kwenye hizo tuhuma na nisingeeleweka kwa
wale niliokuwa naenda kuwapa huduma," alisema.
Askofu Gwajima alisema kuwa baada ya kufika kituoni, alihojiwa na
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam. Kamishna Simon Sirro na
kumweleza kuwa tuhuma dhidi yake zimetokana na chuki.
Alisema alimwomba Kamishna Sirro amruhusu aeleze kwa uhuru kwa kuwa
anayemtuhumu kwa kashfa hiyo, aliwahi pia kumtuhumu Kamanda huyo kwa
kufumbia macho biashara ya uvutaji shisha jijini.
"Lakini Sirro aliniambia kwamba lazima wanihoji na nikamwambia niko
tayari kwa sababu tangu nizaliwe sijawahi kunywa pombe aina yoyote,
kuvuta sigara wala kwenda 'disco'," alisema Askofu Gwajima.
Alisema yuko tayari wampime na hata wakibani ana pombe mwilini mwake, waseme anatumia dawa za kulevya.
Askofu Gwajima alisema kuwa baada ya kuhojiwa, alipelekwa kupimwa kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali na kwamba upimaji uliofanyika huko ulikuwa wa
wazi na anaamini Ofisi ya Rais ilikuwa na wawakilishi katika kupimwa
kwake huko.
Alidai hakubainika kuwa na tatizo katika vipimo hivyo lakini polisi
wakawa wanamhoji kuhusu uhalali wa mali zake ikiwamo ndege na chopa na
kuwajibu kuwa umetokana na huduma ya neno la Mungu.
Aliongeza kuwa, baada ya vipimo hivyo, alikwenda na polisi hadi nyumbani kwake ambako alifanyiwa ukaguzi.
DAWA ZA KULEVYA
Askofu huyo alidai kuwa polisi hawakukuta dawa za kulevya nyumbani kwake
huku akiwaonyesha waumini wake baadhi ya nyaraka za ukaguzi alizodai
kupewa na polisi. Nipashe haikuthibitisha nyaraka hizo, hata hivyo.
"Nyumba yangu ina gorofa tatu, sasa polisi walivyosema wakakague
nyumbani kwangu, niliwaambia twende na tulivyofika watu wote waliokuwa
nyumbani walitoka nje. Kwa hiyo polisi walikagua karatasi kwa karatasi,
dro kwa droo na mpaka kumaliza ilikuwa ni saa nane usiku," alisema.
"Baada ya kukagua na kuona hakukuwa na kitu, niliwaaomba waandike kwamba
hawajakuta kitu, waliandika na nikaomba wanipatie na mimi ‘copy’
(nakala), wakanipatia, hii hapa (alionyesha kanisani).
"Nimepelekwa hadi kwa Mkemia kupimwa na niliwaambia hata wakikuta sigara
au pombe waseme ni dawa lakini kazi ilifanyika kwa uwazi, na baada ya
kupimwa sikukutwa na kitu, walikagua hadi akaunti zangu za benki
hawakukuta kitu.
"Naomba tusiwalaumu polisi, wanafanya kazi ngumu sana na wanateswa kama
sisi, wanaambiwa waende wakakague kwa mtu hata kama hakuna kitu."
Askofu Gwajima alisema Kamanda Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini
(IGP), Ernest Mangu, Mkuu wa Kikosi cha Upelelezi, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali hawapaswi kulaumiwa katika kukamatwa kwake.
Alisema vita dhidi ya dawa za kulevya inapaswa kuungwa mkono lakini
hakubaliani na utaratibu unaotumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
(Makonda).
"Kwa mfano mimi na Makonda huwa tunawasiliana na hata ukiangalia simu
yangu, utaona meseji zake, alishawahi kufika hapa kanisani kwetu tukampa
na kipaza sauti akazungumza, kwanini alishindwa kusema kama tunauza,
naamini anafanya hivi kwa lengo la kuchafua majina ya watu kwa sababu
anazozijua mwenyewe," alisema.
Akizungumzia maisha ya 'selo', Askofu Gwajima alisema hafurahii kuachiwa
kwake kwa sababu amewaacha watu ambao hawana mtu wa kuwasemea na
hawajapimwa wala kukaguliwa kama ilivyofanyika kwake.
Alisema kuwa akiwa selo, alikutana na askari polisi ambao walituhumiwa
katika sakata hilo na anawaonea huruma kwa sababu hawajui hatma yao na
hawana mtu wa kuwatetea.
"Niwaambie kitu, msilaumu polisi wala ofisi ya Rais narudia tena kwa
sababu hawahusiki na hili, isipokuwa ni kiumbe mmoja tu labda na watu
wake wawili watatu ndio wameibuka katikati, polisi nao wanateseka kama
sisi, tangu wametuhumiwa wako ndani mpaka sasa na hakuna wa kuwasaidia,
hawawezi kuzungumza kwa sababu wataonekana ni waasi," alisema.
"Na kwa sababu hiyo, mimi nimejivika rasmi kombati kusema kwa ajili yao.
Namuomba Rais aingilie suala hili maana wanateseka, polisi wamekaa kule
ndani wamejikunyata hawana mtetezi, eti Makonda ameunda tume, hivi kesi
ya ngedere unampelekea nyani?" Alihoji.
DK. WILLIBROD SLAA
Askofu Gwajima pia alidai kutumiwa ujumbe na aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, akieleza
kushtushwa na kuhusishwa na kukamatwa kwake kwa tuhuma za dawa za
kulevya.
Alisoma ujumbe huo kanisani akidai umetumwa kupitia mtandao wa kijamii
wa WhatsApp ambao Dk. Slaa anampa pole kwa kutuhumiwa katika sakata
hilo. Nipashe haikuweza kuthibitisha ujumbe huo kama kweli umetoka kwa
Dk. Slaa.
Katika ujumbe huo, Askofu Gwajima alidai Dk. Slaa alimwambia ameonewa na
haungi mkono utaratibu uliotumika katika kumtuhumu na yuko tayari kutoa
ushahidi juu ya askofu huyo endapo atahitajika kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment