Monday, January 30, 2017

Simba- Manula katunyima pointi tatu

KOCHA msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amemtaja kipa wa Azam FC, Aishi Manula kuwa ndiyo kikwazo cha timu yake kushindwa kupata pointi tatu katika pambano la juzi lililozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa mzunguko wa 19 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba ikiwa nyumbani ilipoteza kwa bao 1-0, na kujiweka katika wakati mgumu kuendelea kubaki kwenye nafasi ya kwanza katika msimamo huo.
Akizungumza baada ya mchezo huo wa juzi Mayanja alisema, Manula aliwakatisha tamaa kabisa baada ya kuokoa nafasi mbili walizozipata dakika za mwishoni kupitia kwa washambuliaji Laudit Mavugo na Pastory Athanas.
“Tunakubali tumepoteza mchezo, Manula alikuwa kikwazo cha sisi kushindwa kupata ushindi, baada ya kuokoa nafasi mbili ambazo tulizipata kupitia kwa Laudit Mavugo na Pastory Athanas, lakini nawapongeza vijana wangu walicheza vizuri kwa muda wote wa mchezo,” alisema Mayanja.
Aidha kocha huyo alisema pamoja na kupokea kipigo hicho bado wanayo nafasi ya ubingwa msimu huu kutokana na ligi kuwa na mechi nyingi mkononi ambazo anaamini wanaweza kucheza na kupata ushindi utakaotimiza ndoto zao za kutwaa ubingwa.
Alisema ni vigumu kuutabiria mpira, lakini bado anaiona nafasi ya ubingwa kwa timu yake ambayo licha ya kupoteza mchezo huo, ina kikosi bora chenye uwezo wa kupambana na kupata matokeo katika kila mechi iliyopo mbele yao.
Kwa upande wa kocha wa Azam, Idd Cheche aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kupata ushindi huo ambao umerudisha ari na matumaini ya kufanya vizuri msimu huu.
Cheche alisema ushindi huo ulitokana na kuisoma vizuri Simba na kubaini mapungufu yao ambapo aliwaeleza wachezaji wake wakati wa mapumziko waliyatumia vizuri na kupata pointi hizo tatu ambazo zimewavuta hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.
Kocha huyo wa muda amekuwa na mafanikio makubwa tangu akabidhiwe timu hiyo mwishoni mwa mwaka jana, akichukua mikoba ya Mhispania Zeben Hernandez ambaye alishindwa kuiongoza vyema timu hiyo.

No comments:

Post a Comment