Tuesday, August 14, 2018

IFAHAMU MIJI BORA NA MIBAYA KUISHI DUNIANI



Mji mkuu wa Austria, Vienna, umeorodheshwa kuwa mji bora zaidi kwa watu kuishi duniani, na kuchukua nafasi ya mji wa Melbourne wa Australia ambao umeongoza kwa miaka mingi.

Mji wa Harare, Zimbabwe ni miongoni mwa miji ambayo haivutii kwa watu kuishi duniani.

Ni mara ya kwanza kwa jiji la bara Ulaya kuongoza kwenye orodha hiyo ya kila mwaka ambayo huandaliwa na Kitengo cha Uchunguzi cha Jarida la Economist.

Utafiti huo uliorodhesha miji 140 duniani kwa kufuata vigezo mbalimbali vikiwemo uthabiti wa kisiasa na kijamii, visa vya uhalifu, elimu na kupatikana kwa huduma bora ya afya.

Katika utafiti huo, jiji la Manchester ndilo lililoimarika zaidi miongoni mwa miji ya Ulaya ambapo jiji hilo lilipanda hatua 16 hadi nafasi ya 35.

Jiji hilo limo mbele ya London kwa hatua 13, ambalo ndilo pengo kubwa zaidi kwa miji hiyo miwili kwenye orodha hiyo tangu kuanza kuandaliwa kwa orodha hiyo miongo miwili iliyopita.

Jarida la Economist limesema kuimarika kwa Manchester ni kwa sababu ya kuimarishwa kwa usalama.

'Ukakamavu'

Utafiti huo ulikosolewa mwaka jana kwa kuushusha hadhi mji wa Manchester baada ya shambulio la Manchester Arena ambapo watu 22 waliuawa.

Mwaka huu, mhariri wa utafiti huo Roxana Slavcheva amesema jiji la Manchester "limenyesha ukakamavu na kujikwamua kutoka kwa shambulio hilo la kigaidi ambalo lilikuwa imetikisa uthabiti wake.

Bi Slavcheva amesema usalama pia umeimarika katika miji kadha ya Ulaya magharibi.

Kuongoza kwa Vienna ni iashara ya kurejea kwa utulivu kiasi katika maeneo mengi ya Ulaya.

Kwa mujibu wa utafiti huo, karibu nusu ya miji imeimarika katika mwaka mmoja uliopita.

Melbourne, ambao kwa sasa ni mji wa pili duniani kwenye orodha hiyo, ilikuwa imeongoza kwa miaka saba mfululizo.

Majiji mengine mawili ya Australia pia yamo kwenye orodha ya kumi bora mwaka huu: Sydney na Adelaide.

Upande ule mwingine, mji mkuu wa Syria, Damascus ambao umeathiriwa sana na vita ndio usiopendwa zaidi na watu duniani ukifuatwa na Dhaka nchini Bangladesh na Lagos nchini Nigeria.

Economist wanasema kwamba uhalifu, machafuko, ugaidi na vita vilichangia sana katika kuorodheshwa chini kwa miji iliyoshika mkia.

Miji bora zaidi kuishi duniani 2018

1. Vienna, Austria

2. Melbourne, Australia

3. Osaka, Japan

4. Calgary, Canada

5. Sydney, Australia

6. Vancouver, Canada

7. Tokyo, Japan

8. Toronto, Canada

9. Copenhagen, Denmark

10. Adelaide, Australia

Miji isiyo bora kuishi duniani 2018

1. Damascus, Syria

2. Dhaka, Bangladesh

3. Lagos, Nigeria

4. Karachi, Pakistan

5. Port Moresby, Papua New Guinea

6. Harare, Zimbabwe

7. Tripoli, Libya

8. Douala, Cameroon

9. Algiers, Algeria

10. Dakar, Senegal

No comments:

Post a Comment