MSHAMBULIAJI hatari wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda amefunguka kuwa anazihofia timu ambazo watakutana nazo kwenye mechi zijazo kwa sababu timu hizo watawapania kwa ajili ya kutaka kuvunja rekodi yao ya kutokufungwa.
Kinara huyo wa mabao ligi kuu amewaongoza Simba kutwaa ubingwa kwa msimu huu lakini pia wakiwa hawajafungwa kwenye mechi zao 28 ambazo wamezicheza hadi sasa huku wakiwa wamebakisha michezo miwili pekee.
Simba inayonolewa na Mfaransa, Pierre Lechantre imebakisha michezo dhidi ya Kagera Sugar ambao wataucheza kwenye Uwanja wa Taifa, Mei 20, kabla ya kwenda kuhitimisha msimu wao ugenini kwa kucheza na Majimaji ya Songea.
akizungumza na Championi Jumatano, Okwi aliyefunga mabao 20 kwenye ligi amesema wanatakiwa kupambana zaidi kwenye mechi hizo mbili kwa ajili ya kutafuta matokeo mazuri kwa sababu wapinzani wao wataingia uwanjani wakiwa na wazo moja la kuwatibulia rekodi yao ya kutokufungwa hadi sasa.
“Kwetu bado hatujamaliza ligi tunatakiwa kupambana zaidi kuhakikisha kwamba tunashinda kwenye mechi hizi ambazo zimebakia, ni muhimu kuendelea kutafuta matokeo mazuri kwa ajili ya kuitunza rekodi ya kutofungwa kwa msimu huu.
“Najua wapinzani wetu wanaofuata Kagera na Majimaji watakuja uwanjani kwa kupania mechi na kucheza kwa nguvu ili tu waweze kututibulia rekodi yetu ya kutofungwa, hivyo itatulazimu sisi kupambana kushinda mechi hizo,” alisema Okwi.
No comments:
Post a Comment