Thursday, May 18, 2017

NDUGU WASUSA MWILI WA MAREHEMU




Dar es Salaam. Zikiwa ni siku nne tangu kuuawa na polisi kwa kupigwa risasi, Salum Almasi akituhumiwa kuwa ni jambazi, ndugu zake hawajamzika wakisema mazingira ya kifo chake yana utata.

Mei 14, nje ya jengo la Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji, Kurasini jijini hapa, Almasi aliuawa akidaiwa pamoja na wenzake walifanya jaribio la kupora fedha wakati gari likizipeleka kwenye mashine ya kielektroniki ya kutolea fedha (ATM) iliyopo kwenye jengo hilo.

Akizungumza jana, msemaji wa familia, Tulleyha Abdulrahman ambaye ni mjomba wa Almasi, alisema utaratibu wa maziko haujakamilika na kwamba, wanashangazwa na tuhuma zinazotolewa dhidi ya ndugu yao kwamba ni jambazi.

Alisema yeye ndiye mlezi wa Almasi ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kituo cha Kompyuta (UCC), akisoma kozi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (IT).

Kabla ya kuuawa, alisema alimwita aende kituo cha basi cha JKT kuchukua fedha za matumizi ya nyumbani ya siku hiyo. “Ushahidi nilivyowasiliana naye upo, mimi ndiye nilimwita pale ilikuwa saa 3:40 asubuhi. Alikuja ingawa alikuwa amenyong’onyea akaniambia macho yanamsumbua, tukakubaliana aende hospitali. Nilimpa Sh30,000 za matumizi ya nyumbani, naambiwa aliuawa saa 3:59 asubuhi binafsi nilipata taarifa za kifo chake saa 10:00 jioni,” alisema.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alipoulizwa iwapo polisi wameshakabidhi mwili wa Almasi kwa familia baada ya uchunguzi, alisema swali hilo wanapaswa kuulizwa watu wa chumba cha kuhifadhia maiti.

No comments:

Post a Comment