Saturday, May 12, 2018

MWIJAGE ADAI UHABA WA SUKARI ILIKUWA NI PROPAGANDA

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema kuadimika kwa bidhaa muhimu ya sukari ilikuwa ni propaganda kwa sababu ipo ya kutosha.

Pia amesema masuala ya propaganda anayafahamu vya kutosha kwa sababu amesomea kutoka China na kufunzwa na mwanasiasa mkongwe marehemu Kingunge Ngombale Mwiru.

Mwijage ametoa kauli hiyo jana  Mei 11 wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala kuhusu bajeti yake kwa mwaka 2018/19 na kuongeza kuwa suala la uhaba wa sukari, yeye ni  mcha Mungu pia aliyekuwa mama yake na bibi walikuwa waislamu hivyo hawezi kuwahujumu Waislamu katika kipindi hiki cha kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Watanzania niwaambie tunayo sukari ya kutosha, kuna tani 45,000 kwenye stoo, Tanzania tunatumia 40,000 kwa mwezi, lakini bandarini nimemwagiza TBS (Shirika la Viwango)  na TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa) sukari iliyopo bandarini itoke. Mbunge wa kwanza ameniambia nimpe tani 1,000. Wabunge njooni mchukue sukari tunayo ya kutosha bandarini tani 22,000 zipo tayari.

“Mbali na sukari hiyo, viwanda vyote vya sukari vimebakisha wiki tatu hadi hadi vianze kuzalisha kwa hiyo suala la uadimikaji wa sukari lilikuwa propaganda na katika propaganda mimi nimesomea mpaka China. Ilikuwa propaganda, sukari ipo, kama ni propaganda, propagandist mwenyewe ni mimi. Kama Mzee Kingunge Ngombale Mwiru mngemuuliza kwa sababu alinifundisha yeye.

“Kwa hiyo hakuna tatizo la sukari, niko hapa na tunafunga kwenye mwezi Mtukufu wa Ramadhani atakayekuwa na tatizo aje aniulize. Tunasambaza sukari kwenda mikoani,” alisema.

No comments:

Post a Comment