Friday, April 27, 2018

NSSF YATAJA AINA YA WANACHAMA LITAKALOWAHUDUMIA

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limetaja aina ya wanachama litakaohudumia baada ya Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kusainiwa na Rais John Magufuli hivi karibuni.

Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke, James Oigo, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waajiri kuhusu sheria hiyo mpya na wajibu wao katika kulinda haki za wanachama.

Watu watakaokuwa wanachama wa NSSF, alisema, ni waajiriwa wote wa sekta binafsi, wageni ambao wameajiriwa Tanzania Bara, waajiriwa katika taasisi za kimataifa zinazofanya kazi Tanzania Bara na watu wote waliojiajiri wenyewe na wale wa sekta isiyo rasmi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya mwaka jana, mifuko ya sekta hiyo imeunganishwa na kubaki miwili - NSSF na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Mifuko iliyounganishwa kwa sheria mpya ni PPF, GEPF, LAPF na PSPF.

Oigo alisema NSSF inawatembelea wanachama wake nchi nzima kuwaelimisha juu ya sheria hiyo, ili kuondoa hofu iliyopo miongoni mwao baada ya mifuko kuunganishwa na kubaki miwili.

Katika ziara hizo, alisema, NSSF itahimiza waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati ili kuliwezesha shirika kulipa mafao ya wanachama kwa ufanisi, kuzijua changamoto zinazowakumba waajiri.

"Waajiriwa wote ambao wataajiriwa baada ya sheria hii kuanza ndio watakuwa katika mfuko ama wa PSSSF endapo wanaajiriwa katika sekta ya umma na NSSF endapo wanaajiriwa katika sekta binafsi," alifafanua.

Aidha, alisema waliokwishaajiriwa wakati sheria hiyo inaanza ambao walikuwa katika mifuko iliyounganishwa watakuwa wanachama wa mfuko wa PSSSF bila kujali wapo setka binafsi au ya umma.

Aidha, watumishi ambao walikuwa wanachama wa NSSF watabakia kuwa wanachama wa NSSF bila kujali sekta wanayotoka, alisema Oigo.

Alizidi kufafanua kuwa kanuni ya ulipaji mafao na idadi ya mafao yatakuwa ya aina moja kwa mifuko yote miwili.

Akifungua mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bathow Mmuni, alisema sheria mpya ya hifadhi ya jamii imeshasainiwa na Rais na sasa zimebakia taratibu za kiuendeshaji.

Naye Meneja wa NSSF Kinondoni, Marco Magheke, alisema shirika limejipanga kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama wake.

No comments:

Post a Comment