Simanzi na vilio vilitawala wakati wa ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa kada wa Chama cha maendeleo na Demokrasia (Chadema), Daniel John, aliyeuawa na watu wasiojulikana.
John aliuawa wiki iliyopita katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, eneo la Coco wakati akitokea katika kampeni za uchaguzi mdogo wa marudio jimbo la Kinondoni na mwili wake uliokotwa katika ufukwe wa Coco.
Wakati mambo yakiwa hivyo katika ibada hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Anna Hananasif, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi liliwazuia wafuasi wa Chadema waliotaka kuusindikiza mwili kwa kuusukuma hadi barabara ya Kawawa Kinondoni.
Ibada ya kuuaga mwili wa John, aliyekuwa Katibu wa chama hicho kata ya Hananasif, ikongozwa na Paroko Alistadius Kibangula, viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, walihudhuria.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu Mwenyekiti Chadema Taifa, Prof. Abdalah Safari, Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.
Akizungumza baada ya ibada, Sumaye alisema chama kimesikitika kwa yote yaliyotokea dhidi ya John.
"Daniel hakufariki (dunia) kwa sababu ya kupigania Chadema, bali alifariki kwa kupigania haki ya Watanzania. Wapo wengi ndani ya Chadema waliofariki dunia kwa kupigania haki,” alisema Sumaye.
Alisema anaamini serikali itafanya uchunguzi pamoja na kutenda haki kwa wote waliohusika na kifo cha Daniel.Naye, Meya Jacob alisema Daniel alikuwa mtaalamu wa siasa za mtaani, na aliishi na watu vizuri.
“Marehemu ndiye aliyechangia ushindi wa Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2015 kwa kupata Diwani na Mbunge. Yeye pia ndiye aliyeisambaratisha CCM kata ya Hananasif iliyokuwa inaongozwa na Tarimba,” alisema Jacob.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi lililazimika kuwazuia wafuasi wa Chadema, waliotaka kuusindikiza mwili wa John.
Baada ya ibada ya kuaga mwili katika Kanisa hilo, wafuasi wa Chadema walijipanga kwa ajili ya kulisindikiza kwa kulisukuma gari lililobeba mwili wa marehemu John lakini walipofika mtaa wa Tarimba eneo la Kinondoni Muslim, walizuiwa na askari waliokuwa kwenye magari mawili ya wazi.
Askari hao walikuwa katika magari yenye namba PT 3675, pamoja na PT 1686 yote aina ya Toyota Land Cruizer. Polisi hao waliwazuia wafuasi hao na gari lililobeba mwili kuendelea na safari.
No comments:
Post a Comment