Sunday, February 11, 2018

NEC:MAANDALIZI YA UCHAGUZI YANAKWENDA VIZURI

Zikiwa zimebaki siku 6 kabla ya Uchaguzi Mdogo wa Majimbo ya Siha, Kinondoni na Kata 8 kufanyika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema maandalizi kwa ajili ya Uchaguzi huo yanaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na ufumbuzi wa changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi RAMADHANI KAILIMA amesema mara baada ya mkutano wa Watendaji wa Tuma na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni Bwana Aron Kagurumujuri.

Bwana Kailima amesema Tume inafuatilia kwa karibu maandalizi ya Uchaguzi Mdogo yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kuwa ni wajibu wake na kwamba Maafisa wa Tume wako maeneo mbalimbali yanayojiandaa kwa Uchaguzi huo Mdogo utakaofanyika jumamosi Februari 17, Mwaka huu.

‘Tumekuja kukutana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ili kupata taarifa juu ya maendeleo ya Maandalizi. Tumekuja hapa kwa sababu hapa ni rahisi kufika’ amesema Bwana Kailima na kuongeza kuwa maafisa wa Tume wapo katika maeneo mbalimbali yanayofanya Uchaguzi kwa kuwa Tume ina wajibu wa kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Uchaguzi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi Tume imejiridhisha kuwa maandalizi yanayoendelea  vizuri na amepongeza jitihada zinazofanywa na Msimamizi wa Uchaguzi pamoja na Wasaidizi wake katika kuhakikisha kuwa changamoto zozote zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Aidha amewashauri Wasimamizi wa Uchaguzi kuendelea kukutana na Wawakilishi wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya kutoa taarifa katika kila hatua ya kuelekea Uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha kuwa Vyama vinapata taarifa ya kila hatua ya maandalizi ili kuwa na uelewa wa pamoja juu ya mchakato mzima wa Uchaguzi.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi amesema Tume imejipanga kuanza kutoa vipindi vya Elimu ya Mpiga Kura mfululizo hadi siku ya Uchaguzi, Elimu itakayohusu mada mbalimbali za Uchaguzi zikiwemo Haki na Wajibu wa Mpiga Kura, Wakala wa Vyama vya Siasa na Msimamizi wa Uchaguzi pamoja na taratibu zote za Upigaji Kura.

‘Nawasihi sana watu watembelee Online ya Tume Tv, website ya Tume, kwa jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi, facebook na instagram lakini pia App ya Tume, kwa hiyo tumeanza Elimu ya namna hiyo kama eneo la kuelimisha Umma kuelekea tarehe 17 siku ya Kupiga Kura’ amesema Bwana Kailima.

Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Majimbo ya Kinondoni mkoani Dar es salaam, Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro na Udiwani katika Kata 8 za Tanzania Bara, unatarajiwa kufanyika Siku ya Jumamosi Februari 17, Mwaka 2018.

No comments:

Post a Comment