Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog.
KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog amesema kuwa baada ya kufanikiwa kuondoka na pointi nne Kanda ya Ziwa, tayari ameanza mikakati ya kuhakikisha timu hiyo inapata ushindi katika mechi zake tatu zijazo ambazo itacheza ndani ya mwezi huu.
Mechi hizo ni dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo itafanyika Oktoba 15, Njombe Mji (Oktoba 21) pamoja na Yanga (Oktoba 27).
Akizungumza na Championi Jumatano, Omog alisema kuwa ushindi atakaoupata katika mechi hizo utaiwezesha Simba kuwa katika nafasi nzuri ya kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ikiwa kileleni jambo ambalo analitamani sana.
Alisema ili lengo lake hilo liweze kutimia atahakikisha anaanza kwa kuifunga Mtibwa Sugar, ambayo iliigomea Yanga Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Uhuru, baadaye Njombe Mji, kisha Yanga ambayo anatamani vijana wake wakiongozwa na Mganda Emmanuel Okwi, waweze kuifunga mabao mengi.
“Hiyo ndiyo mikakati yangu mikubwa kwa sasa baada ya kupata pointi nne Kanda ya Ziwa, pia nimeshawaambia vijana wangu kuwa ni lazima tupate ushindi katika mechi dhidi ya Mtibwa, Njombe na Yanga ili tuweze kumaliza mzunguko wa kwanza tukiongoza.
“Mtibwa ni timu nzuri na hivi karibuni waliigomea Yanga lakini sisi tunataka tuifunge kisha Njombe Mji na baadaye Yanga wenyewe tena kwa mabao mengi,” alisema Omog.
Endapo mipango hiyo ya Omog itafanikiwa basi maisha ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina ndani ya klabu hiyo yatakuwa matatani na anaweza kufungashiwa virago.
Hivi sasa mashabiki wa Yanga hawana tena imani na Lwandamina kutokana na matokeo ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata katika mechi zake zilizopita za ligi kuu na zaidi wamekuwa wakichukuzwa na idadi ndogo ya mabao ambayo imekuwa ikiyafunga.
Katika mechi tano ilizocheza mpaka sasa Yanga imefanikiwa kujikusanyia pointi tisa na mabao manne tu ya kufunga na kufungwa mawili jambo ambalo limeifanya ijikute katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi wakati Simba yenyewe inashika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 11 na mabao 14 ya kufunga na kufungwa matatu.
No comments:
Post a Comment