Wizara ya Afya Zanzibar imepiga marufuku uvutaji sigara kwenye mikusanyiko ya watu ili kuwanusuru watu wasiovuta kuathirika na moshi.
Mkurugenzi Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Jamala Adam Taib, akifungua warsha ya kuimarisha kanuni za kupambana na matumizi ya tumbaku visiwani Zanzibar, alisema uvutaji sigara ni chanzo kikubwa cha ongezeko la maradhi yasiyoambukiza ikiwamo saratani, kisukari, mapafu na homa ya ini.
Alisema licha ya kuwa Zanzibar haizalishi tumbaku na haina viwanda vinavyosarifu bidhaa hiyo, wananchi wanaathirika kwa moshi wa sigara.
Alisema utafiti unaonyesha asilimia kubwa ya watu wanaofariki kutokana na maradhi hayo, chanzo chake ni uvutaji sigara.
Aidha, alisema asilimia 15 ya vifo hivyo vinawafika watu wanaovuta moshi wa sigara zinazovutwa na watu wengine.
“Ili kufanikisha lengo hili nazishauri taasisi za serikali, jumuiya za kiraia na jamii kwa jumla kuunga mkono kanuni inayokataza sigara kuvutwa kwenye mikusanyiko ya watu na kanuni nyingine zinazoundwa ili kulinda afya za wananchi,” alisema.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Ghirmay Andemichael, alisema zaidi ya watu milioni saba, wanapoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku.
Alisema kama hatua hazitachukuliwa za kuandaa mikakati ya kupunguza matumizi ya bidhaa za tumbaku, nusu ya watumiaji wa bidhaa hizo watafariki kwa kuwa tumbaku ni hatari kwa kila mtu na inatabia ya kuua kimya kimya.
Aliishauri serikali, jamii na washirika wa maendeleo kufanya juhudi za ziada kuhakikisha kanuni zinazokataza matumizi ya tumbaku Zanzibar zinaimarishwa na zinatekelezwa kikamilifu.
Aliahidi kuwa WHO itandelea kutoa kila msaada katika kuimarisha kanuni hizo ili kuiwezesha Serikali ya Zanzibar kufikia lengo la maendeleo endelevu la kupunguza vifo vinavyotokana na maradhi yasiyoambukiza kwa asilimia 3.4, ifikapo mwaka 2030.
Akizungumzia Azimio la WHO na mikakati ya kimataifa katika mapambano ya matumizi ya tumbaku, Dk. William Maina, alisema nchi zinapaswa kuongeza kodi ya bidhaa za tumbaku kwa lengo la kuzipandisha bei ili baadhi ya watu washindwe kuzitumia.
Alizitaja njia nyingine kuwa ni kupunguza matangazo ya bidhaa hizo katika vyombo vya habari, kuweka ilani ya madhara ya tumbaku katika vifungashio vya sigara na nchi jirani kushirikiana katika mapambano ya matumizi ya tumbaku.
No comments:
Post a Comment