Saturday, September 16, 2017

TANZANITE KUINGIA KIBARUANI LEO


KOCHA MKUU WA TANZANITE, SEBASTIAN MKOMA.

TIMU ya soka ya Taifa ya vijana ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 (Tanzanite) leo inatupa karata yake ya kwanza kuwavaa wenyeji wao yosso wa Nigeria katika mechi ya kwanza kuwania kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia itakayofanyika kwenye Uwanja wa Samuel Ogbemudian ulioko mjini hapa.

Tanzanite iliwasili mjini hapa jana mchana baada ya juzi kuweka kambi ya muda jijini Abuja.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Tanzanite, Sebastian Mkoma, alisema jana kuwa wachezaji wake wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kuwavaa wapinzani wao licha ya changamoto ya usafiri waliyokutana nayo.

Mkoma alisema kuwa programu yake ya mazoezi waliyoikamilisha wakiwa nchini Tanzania anaiamini itampatia matokeo mazuri na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.

"Tumekuja huku kwa kazi moja ya kulipa deni ambalo Watanzania wametutuma, naamini tutatimiza kile ambacho tumedhamiria katika mechi hii ya ugenini, wachezaji wangu wanajua umuhimu wa kucheza kwa umakini katika dakika zote," alisema Mkoma.

Nahodha wa timu hiyo, Wema Richard, aliliambia gazeti hili kuwa mbali na kujiandaa kuitangaza vyema Tanzania, wachezaji wanataka kujitangaza na kujinadi kwa mawakala wa timu za nje kwa sababu wanajiamini wanauwezo wa kucheza soka la kulipwa.

"Tunamuomba Mungu atusaidie kutimiza ndoto zetu, tushinde mechi ya kesho (leo) na ile tutakayorudiana nyumbani, tunajua hakuna mechi rahisi na hakuna pia kisichowezekana," alisema nahodha huyo.

Mechi hiyo inatarajiwa kuchezeshwa na waamuzi kutoka Togo ambao ni Vicentia Enyonam Amedome, Kossiwa Kpadenou na Abra Sitsope Agbedanou huku Tanzanite ikitarajiwa kuwakaribisha wapinzani wao kati ya Septemba 29 na Oktoba Mosi mwaka huu.

Fainali hizo za wanawake za Kombe la Dunia (U-20) zitafanyika mwakani huko Ufaransa.

No comments:

Post a Comment