Friday, September 15, 2017

RC RUKWA:NATAKA TUWACHOME WAHALIFU"

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu Zelote Stephen aliyevalia kaunda suti.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amefunguka na kudai kukamata na kuchoma nyavu kwa wavuvi haramu haitoshi bali wanapaswa wakamatwe na wachomwe wahalifu hao kwa kutumia sheria ili vitendo hivyo visiweze kujirudia.

Kamishna Mstaafu Zelote amesema hayo wakati akijiandaa kushiriki zoezi la kuteketeza zana haramu zilizokamatwa kupitia doria katika vijiji vya Kabwe, Isaba, Chongokatete, Mandakerenge, Kolwe, Lupata na Kisenga katika wilaya ya Nkasi Mkoani humo, zoezi lililofanyika katika mwalo wa kijiji cha Kirando.

"Kukamata na kuchoma nyavu haitoshi kwa sababu hii inaungua tu, nataka tuwachome wahalifu kwa kutumia sheria. Nimechoma sana nyavu hizi na huu mtindo bado unaendelea, hii haina tija, kila tukichoma madhara yanatokea mazingira yanaharibika. Sasa tuseme basi, ningependa kusikia mhalifu kakamatwa kapelekwa Mahakamani na kupewa adhabu," amesema Kamishna Mstaafu Zelote.

Mhe. Zelote amewaasa watumishi wa idara ya uvuvi ambao wapo chini ya wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini kuachana na kupokea rushwa, kwani jambo hilo linaonekana kukwamisha juhudi za serikali katika kulinda rasilimali zake kwa ajili ya faida ya kizazi hiki na kijacho.

Mhe. Zelote amesema kuwa wananchi bado wanahitaji kuendelea kupatiwa elimu juu ya umuhimu wa kutunza rasilimali na kujulishwa kwamba rasilimali hizo ni za watanzania wote ili waweze kuachana na tabia ya kuvua samaki kwa kutumia zana zisizokubalika.

Kutokana na doria hiyo iliyofanywa na kikosi cha usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kijiji cha Kipili kwa kushirikiana na polisi pamoja na kikosi cha jeshi la wanamaji wote wa kipili kuanzia Juni hadi Septemba 2017 waliweza kukamata nyavu zisizokidhi viwango vya serikali zenye thamani ya shilingi milioni 57.6.

Miongoni mwa nyavu zilizokamatwa ni nyavu 32 za Makira (gilinets) zenye thamani ya shilingi milioni 38.4, nyavu za dagaa zenye macho chini ya 8 mm zenye thamani ya shilingi milioni 16.5 na makokoro ya vyandarua yenye thamani ya shilingi milioni 2.7.

No comments:

Post a Comment