Monday, August 14, 2017

WAZIRI ALIVYOTUA KIWANDANI KININJA

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI, CHARLES MWIJAGE.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alitua alfajiri katika kiwanda cha mafuta ya kula cha Moproco kinachomilikiwa na Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Aziz Abood, imefahamika.

Mwijage, imeelezwa, alifika kiwandani hapo alfajiri kwa lengo la kujionea maandalizi yanayoendelea ya uzalishaji wa mafuta ya alizeti na mashudu.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Meneja Rasilimali Watu wa Abood Seed Oil Industries, Wilson Ndimgwango alisema waziri huyo alifika kiwandani kwake alfajiri ambapo uongozi wa Moproco ukiwa haujaingia kazini.

Hata hivyo, Ndimgwango alisifu staili hiyo ya kuvamia viwanda alfajiri na kumpongeza Waziri Mwijage, akisema anapaswa kuiendeleza, ili kupata uhalisia wa hali ya viwanda ambavyo vilibinafsishwa na serikali na kupewa wawekezaji.

Alisema Waziri Mwijage alifika Moproco saa 12 asubuhi na hakukuta kiongozi kwa kuwa hawakuwa na taarifa ya ujio wake, lakini alijionea shughuli zinazoendelea kwenye kiwanda hicho.

“Hii staili imenifurahisha sana na namwomba aiendeleze kwenye viwanda vingine kwa sababu nina uhakika kwa mtindo huu ataupata ukweli wa kinachoendelea kwenye viwanda vilivyobinafsishwa na serikali,” alisema Ndimgwango.

Akizungumzia hali katika kiwanda hicho, meneja huyo alisema maandalizi yameshakamilika, ikiwamo kununua alizeti ya kutosha kwa ajili ya kuanza uzalishaji.

Mwijage alikipa kiwanda hicho siku 10 kuanzia juzi kuanza uzalishaji, lakini Ndimgwango alisema hazitafika kabla ya kuanza kazi.

“Hata ukija utaona mwenyewe maana mitambo imeshawashwa na kazi zinaendelea," alisema Ndimgwango. "Tunafuatilia vibali Mamlaka ya Chakula na Lishe (TFDA) na Shirika la Viwango Nchini (TBS)."

"Tutakuwa na uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 4,500 hadi 5,000 kwa msimu.”

Alisema kiwanda hicho ambacho tayari kimeshatoa ajira zaidi ya 150, kimeshapata masoko nje ya nchi ambako watauza mashudu na mafuta ghafi.

“Kule kwenye masoko ya nje wengi wanapenda wauziwe mafuta ghafi ili wakasafishe wenyewe, tutawauzia mafuta ghafi, lakini na sisi tumeshafunga mashine, ili mwakani tuanze kuwa tunayasafisha wenyewe hapa hapa nchini.”

VIWANDA 10
Katikati ya wiki iliyopita Mwijage alitangaza viwanda 10 vilivyoshindwa kuzalisha au kuendelezwa baada ya kubinafsishwa, vimefutiwa umiliki wake na ambavyo vitapewa wawekezaji wengine kuvifufua.

Akizungumza mjini Dodoma, Waziri Mwijage alitaja viwanda 10 ambavyo wamepewa wamiliki wengine kutokana na umiliki wa awali kufutwa kuwa ni Kiwanda cha Mkata Saw Mills, Kiwanda cha Korosho Lindi na Kiwanda cha Taifa cha Chuma na Manawa Ginnery.

Vingine ni Kiwanda cha Tembo Chipboard, Mang’ula Mechanical Tools, Mgodi wa Pugu Kaolin, Dabaga Tea Factory, Kiwanda cha Polysack na Kiwanda cha Kilimanjaro Textile Mills cha Arusha.

Hatua ya Mwijage ilikuja siku chache tangu Rais John Magufuli atamke hadharani kuwa waziri huyo anamkwaza kwa kutofuta miliki ya viwanda ambavyo havijaendelezwa kama mwenzake wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Mwijage alisema ubinafsishaji ulihusisha viwanda, mashamba, kampuni za biashara, hoteli na kampuni za usafirishaji zipatazo 431, na kati yake, viwanda vilikuwa 156.

Alisema kati ya viwanda hivyo 156, 62 vinafanya kazi vizuri, 28 vinafanya kazi kwa kusuasua na viwanda 10 vilibinafsishwa kwa kuuzwa mali moja kwa moja.

Alisema katika orodha hiyo, Kiwanda cha Mwanza Tanneries ambacho hakijaendelezwa tangu 1990, mwekezaji wake ameamua kukirudisha serikalini.

No comments:

Post a Comment