Monday, August 21, 2017

SABABU YA SIMBA KUTUA KWA 'MO'

HATIMAYE Simba imepitisha rasmi mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo, huku baadhi ya wanachama wakianika sababu zilizowafanya kuridhia kwa kauli moja mabadiliko hayo katika mkutano wao wa jana.

Wanachama 1,216 kati ya 1,217 waliohudhuria mkutano wa jana uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, walikubali kwa kauli moja mabadiliko ya uwendeshwaji timu hiyo.

Mmoja wa wanachama wa klabu hiyo, Mohamed Isihaka, aliliambia Nipashe kuwa mabadiliko hayakwepeki kwenye timu hiyo kwa kuwa uwendeshwaji wa taasisi za mpira hususan klabu umebadilika na sasa soka ni biashara.

“Kama tunataka maendeleo, lazima tuwaangalie wenzetu wanafanya nini, lazima tuingie kwenye mabadiliko ya mfumo wa uwendeshwaji kibiashara na mimi binafsi nimefurahi kuona hili limefanikiwa,” alisema Isihaka.

Katika mabadiliko hayo yaliyopitishwa jana, wanachama watabaki na umiliki wa asilimia 50 huku asilimia zilizobaki zikitolewa kwa mwekezaji ambaye licha ya kutajwa rasmi jana, Nipashe inafahamu kuwa tayari mfanyabiasha kijana bilionea Mohamed Dewji 'Mo', alishatangaza nia hiyo.

Aidha, mwekezaji huyo atatakiwa kuwekeza Sh. bilioni 20 kumiliki asilimia 50 na wanachama wakitakiwa kuchangia Sh. bilioni nne ambazo ni sawa na asilimia 10.

Asilimia 40 ambazo ni sawa na Sh. bilioni 16 zitawekwa kando kuangalia uwezo wa wanachama hao.

“Suala la nani atakuwa mwekezaji, kamati maalum itaundwa baada ya kupokea maombi ya watu wenye nia ya kuwekeza na baadaye itaamuliwa nani apewe hisa hizo asilimia 50,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.

Alisema endapo watajitokeza wawekezaji wawili au na zaidi, mgawanyo wa hisa utatokana na thamani ya pesa itakayotolewa.

No comments:

Post a Comment