Thursday, August 3, 2017

LIKIZO YA UZAZI KWA KINA BABA YAZUA MJADALA

Hatua ya Serikali kwamba inaangalia uwezekano wa kufuta likizo ya uzazi inayotolewa kwa baba, imeibua mjadala huku makundi ya haki za binadamu na wazazi wakitaka iendelee kutolewa kutokana na umuhimu wake.

Serikali imesema kuwa inafanya uchunguzi ili kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua ya kuifuta au kuiacha baada ya kuwapo madai kuwa baadhi ya kina baba wanaitumia vibaya kwa kwenda baa au katika shughuli nyingine.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili jana kuhusu hilo, walisema Serikali haipaswi kuifuta na badala yake iwaelimishe kina baba umuhimu wa kushirikiana na mama kumlea mtoto mchanga.

“Sidhani kama kuna haja ya kuifuta na jambo la muhimu linalopaswa kufanywa sasa ni Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuelezea umuhimu wa likizo ya uzazi kwa sababu familia zetu nyingi zimetoka katika makuzi yaliyotofautiana,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki na Binadamu(LHRC), Dk Hellen Kijo- Bisimba.

Mtetezi huyo wa haki za binadamu alisema ni kweli baadhi ya kina baba hawakai na wake zao, lakini suala hilo limechangiwa na mambo mengi ikiwamo mila na utamaduni hivyo kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa wahusika.

“Katika baadhi ya familia unaweza kukuta baba akitaka kukaa nyumbani kulea mtoto anafukuzwa kwa hisia kuwa hilo siyo jukumu lake au anataka kumtumikisha mke wake, hivyo njia pekee ya kuondokana na tatizo hilo ni kuendelea kuwapa elimu,” alisema.

Alitaka kina baba waruhusiwe kwenda wodini kushuhudia wake zao wakati wakijifungua hali ambayo itawapa picha halisi kutambua namna mtoto anavyopatikana mbali ya ilivyo sasa wamekuwa watu wa kuhisi tu.

“Hapa mimi ni mwajiri mara zote natoa likizo kwa waajiriwa wangu wakati wake zao wakijifungua na wamekuwa wakitoa msaada mkubwa na ndiyo maana nasisitiza sioni hoja ya kutaka kufuta likizo hii kwani ni ndogo,” alisema.

Hoja ya kupinga kufutwa kwa likizo hiyo pia iliungwa mkono na Hungwi Maliatabu wa mkoani Mwanza aliyejitambulisha kuwa mzazi wa watoto watatu. Mzazi huyo ambaye ni mwalimu wa sekondari alisema Serikali inapaswa kuwamulika wajanja wachache wanaotumia likizo ya uzazi kwa shughuli nyingine na siyo kuifuta.

Alisema likizo hiyo inatoa fursa kwa wazazi wote wawili kufurahia ujio wa mwanafamilia mpya, huku baba akitoa msaada wa kwenda sokoni kusaka mahitaji na kumsaidia mama katika mambo mengine muhimu.

Mama wa watoto watatu aliyejitambulisha kwa jina la Anna Maria alisema wazo la Serikali kuanza uchunguzi kuhusu matumizi mabaya ya likizo hiyo ni jema kwani litasaidia kubaini ukweli, “Iwapo Serikali itabaini kuwa likizo hiyo inatumiwa kinyume na makusudio yake napendekeza ifutwe.”

Alidai kuwa mama anapotoka kujifungua anahitaji mapenzi ya karibu kutoka kwa baba ili kuweza kuijenga afya yake, lakini kuna baadhi ya wazazi licha ya kupewa likizo hiyo hawataki kuwa karibu na wake zao.

No comments:

Post a Comment