Watu watatu wameuawa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab katika eneo la pwani ya Kenya.
Kwa mujibu wa gazeti la Star, Alshabaab walivamia basi hilo la abiria majira ya tisa na nusu alfajiri likisafiri kutoka Mombasa kwenda Kipini.
Vifo hivyo vilitokana na wanamgambo hao kufyatulia risasi kadhaa basi hilo lakini Jeshi la Polisi liliwahi kufika na kujibu mapigo, hali iliyosababisha washambuliaji hao kutokomea kusikojulikana.
Julai 27, Mratibu wa Mkoa wa Pwani, Nelson Marwa alitahadharisha watu wanaofanya safari zao kwa magari binafsi kupitia eneo la Lamu kwenda Mombasa kutofanya hivyo bila kusindikizwa na Jeshi la Polisi.
Alisema kuwa kwa magari ya abiria na ya watu binafsi yatakayojaribu kupita eneo hilo bila kusindikizwa na jeshi la polisi wataadhibiwa ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa leseni zao, kutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha tishio la mashambulizi ya Al-Shabaab.
Kundi la Al-Shabaab ambalo limejikita katika nchi ya Somalia limekuwa likiendesha mashambulizi ya kushtukiza katika baadhi ya maeneo nchini Kenya hususan maeneo ya Pwani.
Aprili mwaka 2015, kundi hilo lilitekeleza shambulizi baya katika Chuo Kikuu cha Garissa lililosababisha watu 148 kupoteza maisha.
No comments:
Post a Comment