Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni limesema tayari limewahoji watu kadhaa kuhusu tukio la jaribio la kulipua nyumba ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Mulilo alisema jeshi hilo hadi sasa linaendelea na uchunguzi ili kubaini kiini cha tukio hilo.
“Hadi sasa tunaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hili na tayari tumewahoji watu kadhaa. Taarifa kamili tutatoa baada ya upelelezi kukamilika,” alisema Kamanda Mulilo.
Agosti 2, mwaka huu, saa 8 usiku, watu wasiofahamika walifanya jaribio la kuchoma moto nyumba ya Sheikh Khalifa ingawa jaribio hilo halikufanikiwa.
Taarifa za Sheikh Khamis anayeishi Magomeni Mtaa wa Lalago zilidai tukio hilo lilidumu zaidi ya nusu saa na ilipofika asubuhi polisi waliwasili katika nyumba hiyo kwa uchunguzi zaidi.
Hata hivyo MTANZANIA lilimtafuta Sheikh Khalifa kwa ajili ya kupata maelezo ya kina kuhusu hali yake na maendelezo kuhusu tukio hilo, lakini hakuweza kupatikana.
No comments:
Post a Comment