Tuesday, July 11, 2017

DIWANI ARUSHA AJIUZULU UANACHAMA CHADEMA NA KUHAMIA CCM

Diwani wa Ngabobo (Chadema), Solomon Laizer ameandika barua ya kujiuzulu udiwani na kujiunga na CCM kwa maelezo anamuunga mkono Rais John Magufuli.

Laizer ni diwani wa tano katika Halmashauri ya Meru kujiuzulu kwa kutoa sababu kuwa anamuunga mkono Rais Magufuli.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Christopher Kazeri amethibitisha jana  (Julai 11) kupata taarifa za kujiuzulu kwa Ngabobo.

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amesema kujiuzulu kwa diwani huyo ni mchezo mchafu akidai  amenunuliwa.

Amesema tayari walipata taarifa za diwani huyo kushawishiwa kujiuzulu na kwamba, alifuatwa na viongozi wa wilaya na kanda wa chama hicho aliowaeleza kuwa ameshawishiwa.

"Baadaye alieleza hataondoka lakini naona wamefanikiwa kumshawishi, tunashangaa viongozi wa Serikali badala ya kufanya kazi za maendeleo wanafanya kazi za kushawishi madiwani wa upinzani kuhama," amesema.

Hata hivyo, madiwani wanaohama wanapinga kuwa wameshawishiwa kufanya hivyo.

Hadi sasa madiwani watano wa Chadema waliojiuzulu ni Credo Kifukwe wa Kata ya Murieti jijini Arusha.

Wengine waliojiuzulu katika Jimbo la Arumeru Mashariki na kata zao kwenye mabano ni Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (Viti Maalumu).

No comments:

Post a Comment