BOGA linalodaiwa kuwa na Sumu limesababisha vifo vya watoto wawili wa familia moja kati ya wanne waliolazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk.Ernest Ibenzi, alithibitisha vifo vya watoto hao.
Alibainisha waliwapokea watoto hao Juni 16, mwaka huu, wakitokea Hospitali ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.
Dk. Ibenzi alisema watoto hao wawili walifariki dunia juzi na jana wakiwa wanapatiwa matibabu katika hospitali hiyo. Alisema watoto hao walipokewa wakiwa wamevimba matumbo, mwili kuwa na njano, kulegea na ini kushindwa kufanya kazi vizuri.
Aliwataja watoto waliofariki dunia kuwa ni Manyari Birika (9) na Taliki Birika (3). Alisema watoto waliobaki wodini ambao wanaendelea na matibabu ni Kitwele Birika (7) na Olijanga Birika (6).
Dk. Ibenzi alisema kutokana na hali hiyo, watachukua vipimo vya damu na ini ili kupeleka haraka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali Dar es Slaam ili kubaini tatizo la ugonjwa unaowasumbua watoto hao.
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya ndani pamoja na sumu kuvu, Dk. Sara Magoma, alisema waliwapokea watoto hao na kuanza matibabu lakini vipimo vimebaini kuwa kuna tatizo kwenye ini kushindwa kufanyakazi vizuri.
Dk. Magoma alitaja sababu za ini kushindwa kufanya kazi vizuri ni vitu vingi ikiwa pamoja na kula kitu chenye sumu ambayo inaweza kushambulia kiungo hicho.
Alisema utafiti unaonyesha mikoa ya Dodoma, Manyara na Singida udongo wake unasumu kuvu ambayo inasababisha mazao yanayolimwa katika maeneo hayo kuwa na sumu hiyo.
No comments:
Post a Comment