MWENYEKITI WA BUNGE, MUSA ZUNGU.
Azimio la Bunge la kumpongeza Rais John Magufuli kwa hatua anazochukua kukabiliana na upotevu wa mapato ya serikali katika sekta ya madini jana liligawa Bunge baada ya wabunge wa upinzani kulikataa wakati wenzao wa CCM wakilikubali.
Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu alipowahoji wabunge kama wanakubali azimio hilo, wabunge wote wa CCM waliitikia "ndiyooo" wakati wale wa upinzani walisema "siyooo".
Azimio hilo lenye kurasa mbili liliwasilishwa bungeni jana na Mbunge wa Newala Mjini (CCM), George Mkuchika na baada ya hapo wabunge walipata nafasi ya kulijadili.
Mbunge wa kwanza kujadili Azimio hilo alikuwa Abdalah Mtolea wa Temeke (CUF), ambaye alisema hakuna haja ya kumpongeza rais kwa kuwa safari bado ni ndefu na matokeo bado hayajaonekana.
Mtolea alisema kuundwa kwa tume mbili za uchunguzi wa usafirshaji mchanga wa madini (makinikia) nje ya nchi si jambo la ajabu wala la kushangilia hivyo ni busara wabunge wakasubiri matunda ya matokeo ya taarifa za tume hizo.
“Waheshimiwa wabunge sijui tunashangilia nini," alisema Mtolea. "Ni mapema mno, Rais wa awamu ya tatu aliunda tume kama hizi, Rais wa awamu ya nne naye aliunda tume kama hizi lakini madini yakaendelea kusafirishwa na tukaendelea kuibiwa. Leo tunashangilia nini sasa?”
Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga alisema Rais Magufuli ameonyesha ujasiri na uzalendo wa hali ya juu kulinda rasilimali za taifa hivyo Azimio la Bunge ni jambo mwafaka kwa wakati huu.
Hasunga alisema Tanzania ina madini mengi ambayo yangeiwezesha Watanzania kuishi maisha mazuri, hivyo hatua alizochukua Rais Magufuli ni lazima ziungwe mkono na watu wote.
Alisema hata marais waliopita walijitahidi kulinda rasilimali kama madini lakini wasaidizi wao ndiyo wanastahili kubebeshwa lawama kwa kushindwa kuwasaidia na kuwashauri vizuri.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugora alisema Watanzania kwa muda mrefu walikuwa wanamwomba Mungu awaletee rais mzalendo na mwenye ujasiri na tayari amepatikana Magufuli.
Lugola alisema Rais Magufuli hata kabla ya kuwa Rais alikuwa akisema kuwa atazuia kusafirishwa kwa mchanga wa dhahabu kwenda nje ya nchi na kwa kuwa ametekeleza, lazima Bunge limpongeze.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema kazi ya wabunge ni kuisimamia na kuishauri serikali na siyo kuisifu hivyo "azimio linalotaka kupitishwa na Bunge halina msingi wowote".
“Mheshimiwa Mwenyekiti hili si azimio la Bunge, hili ni azimio la wabunge wa CCM kumpongeza Mwenyekiti wao wa CCM," alisema Lissu.
"Na kama kweli sisi siyo wanafiki na tunataka kumsifu (Rais) Magufuli basi tuanze kuwasifu marais waliopita maana nao waliwahi kuunda tume kama hizi.”
Aidha, Lissu alisema wakati Watanzania wanaendelea kushangilia kuzuiwa kusafirishwa kwa mchanga, makampuni ya madini yanaendelea kusafirisha madini yanayopatikana hapa nchini na kwamba mikataba yote mibovu bado haijafutwa.
“Alichofanya Rais Magufuli ni sawa na kukataza kusafirisha mapanki (ya samaki) wakati minofu inaendelea kusafirishwa," alisema Lissu.
"Nawahakikishia mpaka leo hii wenye makampuni ya madini wanasafirisha madini, hizi taarifa zote mbili ni za kuwahadaaa tu Watanzania.”
Rais Magufuli alipiga marufuku usafirishaji mchanga nje ya nchi Februari kabla ya kuunda tume mbili ambazo licha ya kugundua uwapo kwa kiasi kikubwa cha madini kwenye makinikia, biashara hiyo imeinyima nchi karibu sh. trilioni 500 katika kodi na mali (madini) tangu mwaka 1998.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, alisema tume alizounda Rais John Magufuli ni tofauti na zile zilizoundwa na marais wastaafu kwa kuwa hizi zimeweka wazi ripoti na tayari rais amechukua hatua.
Lusinde alisema Azimio la Bunge kumpongeza Rais Magufuli limekuja wakati mwafaka kwani marekebisho ya Sheria na Mikataba ni mambo yatakayofuata baadaye kwa kuwa sasa Bunge linajadili Bajeti ya mwaka 2017/2018.
“Mheshimiwa Mwenyekiti ukiona mtu anashindwa kumpongeza aliyefanya vizuri ujue atampongeza mwizi," alisema Lusinde.
"Nawashangaa wabunge wa upinzani kukataa kumpongeza Rais Magufuli wakati (mawaziri wakuu wastaafu walioko Chadema),(Edward) Lowassa na (Fredrick) Sumaye wamempongeza.”
No comments:
Post a Comment