Pia, limesema linamuunga mkono Rais kwa kuwachukulia hatua wafanyakazi wa serikali zaidi ya 9,000 walioghushi vyeti; lakini kwamba linamuomba kuwatazama kwa jicho la huruma wafanyakazi hao, ambao wamesimamishwa kazi kuanzia leo, na kuwasamehe hasa wale waliobakiza miezi michache kustaafu.
Aidha, TUCTA imeomba serikali kuanza kuwachukulia hatua viongozi wa umma wakiwemo wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, wanaowadhalilisha wafanyakazi kwa kuwatolea lugha za matusi na wengine kuwapiga, kwani vitendo hivyo pamoja na kuwavunjia heshima wafanyakazi hao pia vinawapunguzia morali wa kuwajibika. Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa shirikisho hilo mkoa wa Dar es Salaam, George Faustine, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi, iliyoadhimishwa jijini humo kimkoa.
“Hili si suala dogo, ni suala sensitive, kutokana na idadi kubwa ya waliokumbwa na sakata hili. TUCTA hatutetei maovu ila tunathamini utu na heshima ya mtu. Tunaomba serikali iwatizame kwa jicho la huruma wafanyakazi hawa, lakini pia itupie jicho sekta binafsi kwani walioghushi hawapo pekee serikalini,” alisisitiza Faustine. Alisema pamoja na hatua hizo, ni wakati sasa wa serikali kuhakikisha inaandaa mfumo mpya, ambao hautaruhusu tatizo la wafanyakazi wengi kutumia vyeti vya kughushi kukithiri kama ilivyo sasa. Mratibu wa shirikisho hilo wa mkoa wa Dar es Salaam, Musa Mwakalinga, aliiomba serikali kupitia na kuzifanyia kazi changamoto za muda mrefu, zinazowakabili wafanyakazi ili waweze kuwajibika kwa ufanisi na kushiriki katika kukuza uchumi wa taifa hilo.
Alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kutozwa kodi kubwa katika mishahara ya wafanyakazi, huku wafanyakazi hao wakiendelea kununua bidhaa ambazo pia zinatoza kodi na hivyo kuongeza mzigo wa maisha kuwa magumu kwa wafanyakazi hao. Changamoto nyingine ni mishahara na ujira mdogo unaolipwa kwa wafanyakazi wakati gharama za maisha zikiendelea kukua na kutolipwa kwa wakati kwa fedha za mafao ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, jambo linalosababisha wafanyakazi wengi wanapostaafu kucheleweshwa kulipwa mafao yao.
“Katika hili kwenye taasisi za umma hali ndio mbaya zaidi kwani hata mishahara ikipanda, wafanyakazi hawalipwi kwa wakati, jambo linalosababisha kuwepo kwa mlundikano wa malimbikizo,” alisema na kutaja taasisi zinazoongoza kuchelewesha mishahara na kupeleka fedha za mafao kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa ni Tazara na TRL. Kuhusu tatizo la viongozi wa umma wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya, kutoa lugha za matusi kwa wafanyakazi, Mwakalinga alisema baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakidhalilishwa kutokana na lugha chafu wanazotolewa na viongozi hao, tena hadharani na kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya viongozi hao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa TUCTA na Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta aliwataka wafanyakazi kuhakikisha wanajiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuongeza umoja katika kudai haki zao, lakini pia kujiwekea mazingira mazuri ya kufanya kazi. Maadhimisho hayo yalianza kwa maandamano kutoka taasisi, kampuni na mashirika mbalimbali ikiwemo kutangaza bidhaa zao mbele ya wageni waliohudhuria sherehe hizo.
No comments:
Post a Comment