Wednesday, May 17, 2017

UTATA WAIBUKA KUHUSU KIFO CHA MTUHUMIWA WA MAUAJI


KAMANDA WA POLISI MKOA WA KASKAZINI PEMBA, HAJI KHAMISI HAJI.

Mtuhumiwa anayedaiwa kumuua mwanawe kisiwani Pemba alifariki dunia juzi katika mazingira ya kutatanisha akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi.

Mtuhumiwa huyo, marehemu Riziki Juma aliyekuwa mkazi wa Wingwi wilaya ya Micheweni, Pemba alikuwa akidaiwa kumuua mwanawe mchanga pindi baada ya kujifungua Alhamisi iliyopita.

Kufuatia tukio hilo, polisi mkoa wa kaskazini Pemba ilikuwa inawashikilia watu watatu, akiwemo marehemu Riziki ambaye ndiye mama mzazi, baba wa mtoto na mzazi wa kike wa baba huyo.

Wakati Jeshi la Polisi likisema mtuhumiwa huyo alifariki akiwa hospitalini, daktari aliyempokea hospitalini aliiambia Nipashe kuwa alipompokea kutoka mikononi mwa polisi akiwa ameshafariki dunia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji Khamisi Haji alisema waliamua kumpelaka mtuhumiwa huyo hospitali baada ya kusema kuwa anaumwa na anahitaji kupatiwa matibabu.

Hata hivyo, daktari aliyemfanyanyia uchunguzi marehemu huyo, Dk. Khalifan Said Salum alisema walimpokea mwanamke huyo akiwa ameshafariki dunia.

“Wakati tunaendelea kumpima marehemu tulimkuta akiwa ametokwa na povu jingi mdomoni na hivi sasa tumechukuwa sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili tujuwe chanzo cha kifo chake,” alisema Dk. Salum.

Marehemu alikuwa akituhumiwa kumuua mtoto wake ili kuficha aibu, baada ya kujifungua ndani ya mwezi mmoja baada ya kuolewa.

No comments:

Post a Comment