Bunge limeitaka serikali iharakishe mchakato wa kufanya uamuzi wenye tija ili kuokoa gharama ambazo inaingia kwa kumtunza Faru Fausta.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye, alitoa ushauri huo alipowasilisha bungeni mjini hapa jana taarifa ya kamati yake kuhusu makadiio ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka ujao wa fedha.
Alisema faru huyo amewekwa katika uangalizi maalum kutokana na maradhi aliyo nayo na umri wake.
Aprili 6, ikiwa siku ya tatu tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti, Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul, alilieleza Bunge kuwa Hifadhi ya Ngorongoro inatumia Sh. milioni 64 kwa mwezi, sawa na Sh. milioni 768 kwa mwaka, kumlisha na kumtunza Faru Fausta.
Baada ya mbunge huyo kuhoji bungeni matumizi hayo makubwa kumtunza faru huyo, serikali kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, ilitoa maelezo ikikiri kutunzwa gharama hizo kubwa ilizodai zinatokana na kumlisha chakula na ulinzi kwa kuwa ni mzee.
Prof. Maghembe alisema mnyama huyo pia ananyemelewa na magonjwa mbalimbali ndiyo maana ana gharamiwa kwa kiasi hicho kikubwa cha fedha.
Aidha, waziri huyo alisema wanafanya hivyo pia kwa sababu wanyama wa aina hiyo ni wachache katika hifadhi hiyo.
Katika taarifa ya kamati yake jana, Mhandisi Nditiye pia aliishauri serikali kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya ukarabati wa maeneo ya makumbusho ya Taifa, kuanisha vivutio vya malikale na kuviendeleza, kutatua migogoro iliyopo kati ya hifadhi za misitu na jamii, kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya mkaa na kupanda miti na kuongeza juhudi na mbinu za kisasa katika kutokomeza ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.
Kamati hiyo pia iliishauri serikali kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori walio hatarini kutoweka kama faru na tembo, kuhamisisha sekta binafsi katika kuboresha hoteli pamoja na kuongeza kasi ya uwekezaji kikamilifu katika miundombinu ya maji, barabara na vyoo kama ilivyofanya kwa viwanja vya ndege.
No comments:
Post a Comment