Wednesday, May 24, 2017

IDADI YA WANAOJIUNGA JKT YAPUNGUA


Bunge limeelezwa kuwa takwimu zinaonyesha idadi ya vijana wanaojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, inapungua kila mwaka.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, aliliambia bunge wakati akijibu swali la Mbunge wa Newala Mjini (CCM), George Mkuchika.

Mkuchika alitaka kujua katika miaka  mitatu iliyopita vijana wangapi walijiunga na mafunzo ya JKT na waliojiunga ni asilimia ngapi ya wanaotakiwa kujiunga.
Akijibu swali hilo, Dk.Mwinyi alisema kupungua kwa idadi hiyo kumesababishwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kugongana kwa tarehe za kuanza mafunzo ya vijana wa mujibu wa sheria na kufunguliwa kwa vyuo mbalimbali nchini.
“Hali hii imewafanya vijana wengi walioteuliwa kujiunga na vyuo kukosa nafasi ya kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Alitaja changamoto nyingine ni uhaba wa miundombinu, rasilimali watu na fedha na kwamba serikali inaendelea na juhudi za kupata suluhu ya changamoto zilizopo.
Alifafanua Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa (1964) imeweka ulazima wa vijana wa Tanzania wanaomaliza Kidato cha Sita kujiunga na mafunzo ya JKT, kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, alisema mwaka 1994 serikali iliyasitisha kwa muda mafunzo hayo na kuyarejesha tena mwaka 2013 na yameendelea kutolewa hadi sasa.
 Alitaja takwimu za vijana waliohitimu kidato cha sita na kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa kipindi cha mwaka 2014 vijana waliohitimu kidato cha sita walikuwa 41,968 kati yao waliojiunga ni 31,692 sawa na asilimia 75.5.
Aidha, Katika kipindi cha mwaka 2015 vijana waliohitimu kidato cha sita walikuwa 40,753 kati yao waliojiunga ni 19,990 sawa na asilimia 48.8.
“Mwaka 2016, vijana waliohitimu kidato cha sita walikuwa 63,623 kati yao waliojiunga ni 14,747 sawa na asilimia 23.2,”alisema

No comments:

Post a Comment